Skip to content

Matendo 2

Kushuka Kwa Roho Mtakatifu

1Ilipowadia siku ya Pentekoste, walikuwa wote mahali pamoja. 2Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo uliotoka mbinguni, ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. 3Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao. 4Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.
5Basi walikuwepo Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu. 6Waliposikia sauti hii, umati wa watu ulikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. 7Wakiwa wameshangaa na kustaajabu wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya? 8Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa? 9Warparthi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto na Asia, 10Frigia, Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene na wageni kutoka Rumi, 11Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu, sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.” 12Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?”
13Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa mvinyo!”

Petro Ahutubia Umati

14Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na moja, akainua sauti yake na kuhutubia ule umati wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, jueni jambo hili mkanisikilize. 15Hakika watu hawa hawakulewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi! 16Hawa hawakulewa, ila jambo hili ni lile lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema: 17“ ‘Katika siku za mwisho, asema Bwana,
nitamimina Roho wangu
juu ya wote wenye mwili.
Wana wenu na binti zetu watatabiri,
vijana wenu wataona maono
na wazee wenu wataota ndoto.
18Hata juu ya watumishi wangu
nitamwaga Roho wangu,
nao watatabiri.
19Nami nitaonyesha maajabu mbinguni juu
na ishara duniani chini, damu,
moto na mvuke wa moshi mnene.
20Jua litakuwa giza
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana
iliyo tukufu.
21Lakini ye yote atakayeliita
jina la Bwana, ataokolewa.’
22“Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kwa kupitia yeye, kama ninyi wenyewe mjuavyo. 23Huyu mtu akiisha kutolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimwua kwa kumgongomea msalabani. 24Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti. 25Kwa maana Daudi asema kumhusu yeye:“ ‘Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote.
Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,
sitatikisika.
26Kwa hiyo moyo wangu unafurahia
na ulimi wangu unashangilia;
mwili wangu nao utaishi kwa tumaini.
27Kwa maana hutaniacha kaburini,
wala hutamwacha
aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.
28Umenionyesha njia za uzima,
utanijaza na furaha mbele zako.’

29“Ndugu zangu Waisraeli, nataka niwaambie kwa uhakika kwamba baba yetu Daudi alikufa na kuzikwa, nalo kaburi lake lipo hapa mpaka leo. 30Lakini alikuwa nabii na alijua ya kuwa Mungu alikuwa amemwahidi kwa kiapo kwamba angemweka mmoja wa wazao wake penye kiti chake cha enzi. 31Daudi akiona mambo yaliyoko mbele, akanena juu ya kufufuka kwa Kristo , kwamba hakuachwa kaburini, wala mwili wake haukuona uharibifu. 32Mungu alimfufua huyu Yesu na sisi sote ni mashahidi wa jambo hilo. 33Basi ikiwa yeye ametukuzwa kwa mkono wa kuume wa Mungu, amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia. 34Kwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema,“ ‘BWANA alimwambia Bwana wangu:
“Keti upande wangu wa kuume,
35hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.” ’

36“Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulibisha, kuwa Bwana na Kristo.”

Ongezeko La Waamini

37Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”
38Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. 39Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu na kwa wale wote walio mbali na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”
40Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.” 41Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.

Ushirika Wa Waamini

42Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, wakamgawia kila mtu kwa kadiri alivyokuwa anahitaji. 46Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa kwa wale watu waliokuwa wakiokolewa. Matendo 2:1_47