Skip to content

Kutoka 12:1-42

Pasaka

1BWANA akamwambia Mose na Aroni katika nchi ya Misri, 2“Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu, yaani mwezi wa kwanza wa mwaka wenu. 3Iambie jumuiya yote ya Israeli kwamba katika siku ya kumi ya mwezi huu, kila mtu atatwaa mwana-kondoo mmoja kwa ajili ya familia yake, mmoja kwa kila nyumba. 4Ikiwa nyumba yo yote ina watu wachache wasioweza kumaliza huyo mwana-kondoo mzima, nyumba hiyo itabidi ishirikiane na nyumba ya jirani wa karibu, baada ya kuzingatia idadi ya watu waliomo. Mtaangalia ni kiasi gani cha nyama kitahitajika kulingana na mahitaji ya kila mtu. 5Wanyama mtakaowachagua, lazima wawe wa kiume wa umri wa mwaka mmoja wasio kuwa na dosari, mwaweza kuwachukua kati ya kondoo au mbuzi. 6Tunzeni wanyama hao mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi, ambapo lazima watu wa jumuiya yote ya Israeli wachinje wanyama hao wakati wa jioni. 7Ndipo watakapochukua baadhi ya hiyo damu na kuipaka kwenye vizingiti vya juu na miimo ya milango ya nyumba ambamo watakula wana-kondoo hao. 8Usiku huo huo watakula nyama iliyookwa kwenye moto, pamoja na mboga chungu za majani na mikate isiyotiwa chachu. 9Msile nyama mbichi wala iliyochemshwa, lakini iwe imeokwa kwenye moto, kichwa, miguu na nyama zake za ndani. 10Msibakize nyama yo yote mpaka asubuhi; nazo kama zitabakia mpaka asubuhi, lazima mziteketeze kwa moto. 11Hivi ndivyo mtakavyokula: Mtajifunga mikanda viunoni, mtakuwa mmevaa viatu vyenu miguuni na kushika fimbo zenu mkononi mwenu. Mle kwa haraka; hii ni Pasaka ya BWANA.
12“Usiku uo huo nitapita katika nchi yote ya Misri na kumwua kila mzaliwa wa kwanza, wa wanadamu na wa wanyama, nami nitaihukumu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi BWANA. 13Damu itakuwa ishara kwa ajili yenu ya kuonyesha nyumba ambazo mtakuwamo; nami nitakapoiona damu, nitapita juu yenu. Hakuna pigo la uharibifu litakalowagusa ninyi nitakapoipiga Misri.
14“Siku hii itakuwa kumbukumbu kwenu; mtaiadhimisha kuwa sikukuu kwa BWANA, katika vizazi vyenu vyote: mtaishika kuwa amri ya kudumu. 15Kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza mtaondoa chachu yote ndani ya nyumba zenu, kwa maana ye yote atakayekula cho chote chenye chachu kuanzia siku ya kwanza hadi ya saba lazima akatiliwe mbali kutoka katika Israeli. 16Katika siku ya kwanza mwe na kusanyiko takatifu, na kusanyiko jingine katika siku ya saba. Katika siku hizo msifanye kazi kamwe isipokuwa kutayarisha chakula cha kila mmoja; hilo ndilo tu mtakalofanya.
17“Mtaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, kwa sababu hiyo ndiyo siku ile niliyovitoa vikosi vyenu kutoka Misri. Mtaiadhimisha siku hii kwa vizazi vyenu vyote kuwa amri ya kudumu. 18Katika mwezi wa kwanza mtakula mikate isiyotiwa chachu, kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne hadi jioni ya siku ya ishirini na moja. 19Kwa muda wa siku saba isionekane chachu yo yote katika nyumba zenu. Ye yote alaye cho chote chenye chachu ndani yake, lazima akatiliwe mbali kutoka katika jumuiya ya Israeli, akiwa ni mgeni au mzawa. 20Msile cho chote kilichotiwa chachu. Po pote muishipo, ni lazima mle mikate isiyotiwa chachu.”
21Ndipo Mose akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, “Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka. 22Chukueni kitawi cha hisopo, kichovyeni kwenye damu iliyopo kwenye sinia na kuipaka baadhi ya hiyo damu kwenye vizingiti na kwenye miimo yote miwili ya milango. Mtu ye yote asitoke nje ya mlango wa nyumba yake mpaka asubuhi. 23BWANA apitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu juu ya vizingiti na kwenye miimo ya milango, naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwapiga ninyi.
24“Shikeni maagizo haya kuwa kanuni ya kudumu kwenu na kwa ajili ya wazao wenu. 25Mtakapoingia katika nchi BWANA atakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii. 26Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’ 27Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwa BWANA, ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ” Ndipo watu wa Israeli waliposujudu na kuabudu. 28Waisraeli wakafanya kama vile BWANA alivyomwagiza Mose na Aroni.
29Ilipofika usiku wa manane, BWANA akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika Misri, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa, aliyekuwa gerezani, na wazaliwa wa kwanza wa mifugo yote pia. 30Farao, na maafisa wake wote, na Wamisri wote wakaamka usiku, na kulikuwa na kilio kikubwa katika nchi ya Misri, kwa kuwa haikuwepo nyumba ambayo hakufa mtu.

Kutoka

31Wakati huo Farao akawaita Mose na Aroni na kuwaambia, “Ondokeni! Tokeni katika watu wangu, ninyi pamoja na Waisraeli! Nendeni mkamwabudu BWANA kama mlivyoomba. 32Chukueni makundi yenu ya kondoo na mbuzi pamoja na ng’ombe, kama mlivyosema, nanyi mwende zenu. Nanyi pia mnibariki.”
33Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke kwa haraka na kuacha nchi yao. Kwa kuwa walisema, “La sivyo, tutakufa wote!” 34Hivyo watu wakachukua donge lao la unga kabla ya kutiwa chachu, wakaweka ndani ya mabakuli ya kukandia, wakayaviringisha katika vitambaa na kuyabeba mabegani mwao. 35Waisraeli wakafanya kama Mose alivyowaelekeza, nao wakawaomba Wamisri wawapatie vitu vya fedha, dhahabu na nguo. 36Basi BWANA alikuwa amewafanya Wamisri kuwa wakarimu kwa hawa watu, wakawapatia Waisraeli vile walivyotaka kwao; kwa hiyo wakawateka nyara Wamisri.
37Waisraeli wakasafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi. Walikuwepo wanaume wapatao 600,000 waendao kwa miguu bila kuhesabu wanawake na watoto. 38Watu wengine wengi wakafuatana nao, pamoja na makundi makubwa ya mifugo wakiwemo kondoo, mbuzi na ng’ombe. 39Wakatengeneza maandazi yasiyotiwa chachu kwa ule unga uliokandwa waliokuwa wameutoa Misri, donge hilo la unga halikuwa limetiwa chachu, kwa kuwa walikuwa wameondolewa Misri kwa haraka nao hawakuwa na muda wa kuandaa chakula chao.
40Waisraeli walikuwa wameishi Misri kwa muda wa miaka 430. 41Ilikuwa ni siku ya mwisho ya hiyo miaka 430, vikosi vyote vya BWANA vilipokuwa vimeondoka Misri. 42Kwa sababu BWANA aliutenga usiku ule ili kuwatoa Waisraeli katika nchi ya Misri, katika usiku huu Waisraeli wote wanapaswa kuadhimisha kwa kukesha ili kumheshimu BWANA katika vizazi vijavyo.