Skip to content

Ishara ya Adam – Qur’an

Ishara ya Adam – Taurati

(Miinuko) Surat 7:19-26

Na wewe, Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani hii, na kuleni humo mpendapo. Wala msiukaribie mti huu, mkawa katika wale walio dhulumu.

Basi Shet’ani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizo fichiwa, na akasema: Mola Mlezi wenu hakukukatazeni mti huu ila msije mkawa Malaika, au msije mkawa katika wanao ishi milele.”

Naye akawaapia: Kwa yakini mimi ni miongoni wa wanao kunasihini.

Basi akawateka kwa khadaa. Walipo uonja ule mti, tupu zao zilifichuka na wakaingia kujibandika majani ya Bustanini. Mola wao Mlezi akawaita: Je, sikukukatazeni mti huo, na kukwambieni ya kwamba Shet’ani ni adui yenu wa dhaahiri?

Wakasema: Mola wetu Mlezi! tumejidhulumu nafsi zetu, na kama hutusamehe na kuturehemu, hakika tutakuwa katika wenye kukhasirika.

Akasema: Teremkeni! Mtakuwa nyinyi kwa nyinyi maadui. Na kwenye ardhi itakuwa ndio makao yenu na starehe yenu mpaka ufike muda.

Akasema: Humo mtaishi, na humo mtakufa, na kutoka humo mtatolewa.

Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na nguo za pambo. Na nguo za uchamngu ndio bora. Hayo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu mpate kukumbuka.

(Ta Ha) Surat 20: 121-123

Basi wakaula wote wawili, na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustani. Na Adam akamuasi Mola wake Mlezi, na akapotea njia.

Kisha Mola wake Mlezi akamteuwa, naye akamkubalia toba yake, naye akamwongoa.

Akasema: Ondokeni humu nyote, hali ya kuwa ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Na ukikufikieni uwongofu kutoka kwangu basi atakaye ufuata uwongofu wangu, hatapotea wala hatataabika.

Mwanzo 2:15-17

15BWANA Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza. 16BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akamwambia, “Uko huru kula matunda ya mti wo wote katika bustani, 17lakini kamwe usile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa.”

Mwanzo 3:1-23

1Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao BWANA Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wo wote wa bustanini’?”
2Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini, 3lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala msiguse kabisa, la sivyo mtakufa.’ ”
4Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. 5Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
6Mwanamke alipoona ya kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala. 7Ndipo macho yao wote wawili yakafumbuliwa, wakajiona kwamba walikuwa uchi; hivyo wakashona majani ya mtini, wakajifunika.
8Ndipo yule mwanaume na mkewe, waliposikia sauti ya BWANA Mungu alipokuwa akitembea bustanini wakati wa utulivu wa jioni, wakajificha kutoka mbele za BWANA Mungu katikati ya miti ya bustani. 9Lakini BWANA Mungu akamwita Adamu, “Uko wapi?”
10Naye akajibu, “Nilikusikia katika bustani nikaogopa kwa sababu nilikuwa uchi, hivyo nikajificha.”
11Mungu akamwuliza, “Ni nani aliyekuambia yakuwa ulikuwa uchi? Je, umekula matunda ya mti niliokuamuru usile?”
12Adamu akasema, “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa sehemu ya tunda kutoka kwenye huo mti, nami nikala.”
13Ndipo BWANA Mungu akamwuliza mwanamke, “Ni nini hili ambalo umelifanya?” Mwanamke akajibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”
14Hivyo BWANA Mungu akamwambia nyoka, “Kwa kuwa umefanya hili,“Umelaaniwa kuliko wanyama wote
wa kufugwa na wa porini!
Utatambaa kwa tumbo lako
na kula mavumbi
siku zote za maisha yako.
15Nami nitaweka uadui
kati yako na huyo mwanamke,
na kati ya uzao wako na wake,
huo atakuponda kichwa,
nawe utamgonga kisigino.”

16Kwa mwanamke akasema,“Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;
kwa utungu utazaa watoto.
Tamaa yako itakuwa kwa mumeo
naye atakutawala.”

17Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’“Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako,
kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo
siku zote za maisha yako.
18Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako,
nawe utakula mimea ya shambani.
19Kwa jasho la uso wako
utakula chakula chako
hadi utakaporudi ardhini,
kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo,
kwa kuwa wewe u mavumbi
na mavumbini wewe utarudi.”

20Adamu akamwita mkewe Eva, kwa kuwa atakuwa mama wa wote walio hai.
21BWANA Mungu akawatengenezea Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. 22Kisha BWANA Mungu akasema, “Sasa mtu huyu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya. Sharti asiruhusiwe kunyosha mkono wake na kuchuma pia kutoka katika mti wa uzima akala, naye akaishi milele.” 23Hivyo BWANA Mungu akamfukuzia mbali kutoka Bustani ya Edeni, akalime ardhi ambamo alitolewa. 24Baada ya kumfukuzia mbali Adamu, Mungu akaweka makerubi mashariki ya Bustani ya Edeni, pamoja na upanga wa moto ukimulika huku na huko kulinda njia ya kuuendea mti wa uzima.