Skip to content

Surat 5:28-31 (Maida)

Mwanzo 4:1-12

Ukininyooshea mkono wako kuniuwa, mimi sitakunyooshea mkono wangu kukuuwa. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.

Mimi nataka ubebe dhambi zangu na dhambi zako, kwani wewe utakuwa miongoni mwa watu wa Motoni. Na hayo ndiyo malipo ya wenye kudhulumu.

Basi nafsi yake ikampelekea kumuuwa nduguye, akamuuwa na akawa miongoni mwa wenye kukhasirika.

Hapo Mwenyezi Mungu akamleta kunguru anaye fukua katika ardhi ili amwonyeshe vipi kumsitiri nduguye. Akasema: Ole wangu! Nimeshindwa kuwa kama kunguru huyu nikamsitiri ndugu yangu? Basi akawa miongoni mwa wenye kujuta.

Kaini Na Abeli

1Adamu akakutana kimwili na mkewe Eva, akapata mimba, akamzaa Kaini. Eva akasema, “Kwa msaada wa BWANA nimemzaa mwanaume.” 2Baadaye akamzaa Abeli ndugu yake.
Basi Abeli akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima.
 3Baada ya muda Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba kama sadaka kwa BWANA. 4Lakini Abeli akaleta fungu nono kutoka katika baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. BWANA akamkubali Abeli pamoja na sadaka yake, 5lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni.
6Kisha BWANA akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? 7Ukifanya lililo sawa, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.”
8Basi Kaini akamwambia ndugu yake Abeli, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamwua.
9Kisha BWANA akamwuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?”
Akamjibu, “Sijui, je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
10BWANA akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. 11Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka katika ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako. 12Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani asiye na utulivu.”