Skip to content

Ndoto Za Yosefu

1Yakobo akaishi Kanaani katika nchi ambayo baba yake alikuwa ameishi.
2Zifuatazo ni habari za Yakobo.
Yosefu, kijana wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga makundi ya kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake wa mama wengine, yaani wana wa Bilha na wana wa Zilpa wake za baba yake, naye akawa akimletea baba yake taarifa mbaya kuhusu hao ndugu zake.3Basi, Israeli akampenda Yosefu kuliko ye yote miongoni mwa kaka zake, kwani ni mwanawe wa uzeeni, akamshonea joho lililorembwa vizuri sana. 4Ndugu zake walipoona kwamba baba yao anampenda Yosefu kuliko ye yote mwingine miongoni mwao, walimchukia na hawakusema naye neno lo lote jema.
5Yosefu akaota ndoto, naye alipowaeleza ndugu zake, wakamchukia zaidi. 6Akawaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota: 7Tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani, ghafula mganda wangu ukasimama wima, wakati miganda yenu ikiuzunguka na kuuinamia.”
8Ndugu zake wakamwambia, “Wewe unakusudia kututawala? Hivi kweli wewe utatutawala sisi?” Wakaongeza kumchukia zaidi kwa sababu ya ndoto yake pamoja na yale aliyowaambia.
9Kisha akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine, wakati huu jua, mwezi na nyota kumi na moja zilikuwa zinanisujudia.”
10Alipomwambia baba yake pamoja na ndugu zake, baba yake akamkemea akisema, “Ni ndoto gani hii uliyoota? Hivi kweli mama yako na mimi na ndugu zako tutakuja kukusujudia wewe hadi nchi?” 11Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akaliweka jambo hilo moyoni.

Yosefu Anauzwa Na Ndugu Zake

12Basi, ndugu zake walikuwa wamekwenda kuchunga makundi ya baba yao karibu na Shekemu, 13naye Israeli akamwambia Yosefu, “Kama ujuavyo, ndugu zako wanachunga makundi huko karibu na Shekemu. Njoo, nitakutuma kwao.”
Yosefu akajibu, “Vema sana niko tayari.”14Kwa hiyo akamwambia, “Nenda uone kama mambo yote ni salama kwa ndugu zako na makundi, kisha uniletee habari.” Ndipo akamtuma Yosefu kutoka Bonde la Hebroni.
Yosefu alipofika Shekemu, 15mtu mmoja akamkuta akizungukazunguka mashambani na akamwuliza, “Unatafuta nini?”
16Akajibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Unaweza kuniambia wanachunga wapi makundi yao?”
17Yule mtu akajibu, “Wamehama hapa. Nimesikia wakisema, ‘Twende Dothani.’ ”
Kwa hiyo Yosefu akawafuatilia ndugu zake na kuwakuta karibu na Dothani. 18Ndugu zake walipomwona akiwa mbali, kabla hajawafikia, wakapanga shauri baya la kumwua.
19Wakaambiana, “Yule mwota ndoto anakuja! 20Njoni sasa, tumwue na kumtupa katika shimo mojawapo na tuseme kwamba mnyama mkali amemrarua. Kisha tutaona matokeo ya ndoto zake.”
21Reubeni aliposikia jambo hili, akajaribu kumwokoa kutoka mikononi mwao akasema, “Tusiutoe uhai wake. 22Tusimwage damu yo yote. Mtupeni katika shimo lililoko hapa jangwani, lakini msimguse.” Reubeni alisema hivyo ili amwokoe kutoka mikononi mwao, kisha amrudishe nyumbani kwa baba yake.
23Kwa hiyo Yosefu alipowafikia ndugu zake, walimvua lile joho lake, lile joho lililorembwa vizuri alilokuwa amevaa. 24Kisha wakamchukua wakamtupa katika shimo. Wakati huo shimo lilikuwa tupu, halikuwa na maji ndani yake.
25Walipokaa ili wale chakula chao, wakainua macho wakaona msafara wa Waishmaeli ukija kutoka Gileadi. Ngamia wao walikuwa wamepakizwa mizigo ya vikolezo, uvumba na manemane, nao walikuwa njiani kuvipeleka Misri.
26Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutafaidi nini ikiwa tutamwua ndugu yetu na kuificha damu yake? 27Njoni, tumwuze kwa hawa Waishmaeli, tusimguse kwa kuwa hata hivyo, yeye ni ndugu yetu, nyama yetu na damu yetu wenyewe.” Ndugu zake wakakubali.
28Kwa hiyo wale wafanyabiashara Wamidiani walipofika pale, ndugu zake wakamtoa Yosefu kutoka kwenye lile shimo na kumwuza kwa shekeli ishirini  za fedha kwa wale Waishimaeli, ambao walimpeleka Misri.
29Reubeni aliporudi kutazama kwenye lile shimo na kuona kwamba Yosefu hayupo, alirarua nguo zake. 30Akawarudia ndugu zake na kusema, “Kijana hayuko mle! Nielekee wapi sasa?”
31Kisha wakalichukua lile joho la Yosefu, wakachinja mbuzi na kulichovya katika damu. 32Wakalichukua lile joho lililorembwa vizuri na kulipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeliokota hili joho. Uchunguze uone kama ni la mwanao.”
33Baba yao akalitambua akasema, “Hili ni joho la mwanangu! Mnyama mkali amemrarua. Hakika Yosefu ameraruliwa vipande vipande.”
34Kisha Yakobo akararua nguo zake, akavaa nguo ya gunia na kumwombolezea mwanawe kwa siku nyingi. 35Wanawe wote na binti zake wakaja kumfariji, lakini hakukubali kufarijiwa. Akasema, “Hapana, nitamwombolezea mwanangu mpaka nimfikie kaburini.” Kwa hiyo baba yake akaendelea kumlilia.
36Wakati ule ule, Wamidiani wakamwuza Yosefu huko Misri kwa Potifa, mmojawapo wa maafisa wa Farao, aliyekuwa mkuu wa ulinzi.

Yosefu Na Mke Wa Potifa

1Wakati huu Yosefu alikuwa amechukuliwa mpaka Misri. Mmisri aliyeitwa Potifa aliyekuwa mmojawapo wa maafisa wa Farao, mkuu wa ulinzi, akamnunua Yosefu kutoka kwa Waishimaeli waliomleta Misri.
2BWANA alikuwa pamoja na Yosefu, naye akastawi, Yosefu akaishi nyumbani kwa bwana wake Mmisri. 3Potifa alipoona kuwa BWANA alikuwa pamoja na Yosefu na kwamba BWANA alimfanikisha kwa kila kitu alichokifanya, 4Yosefu alipata kibali machoni pa Potifa, akamfanya mhudumu wake. Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, naye akamkabidhi kuwa mwangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho. 5Kuanzia wakati huo Potifa alipomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba na mali zake zote alizokuwa nazo, BWANA aliibariki nyumba ya Potifa kwa sababu ya Yosefu. Baraka ya BWANA ilikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa, nyumbani na shambani. 6Kwa hiyo Potifa akamwachia Yosefu uangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho, Yosefu alipokuwa katika uongozi, Potifa hakuwa na sababu ya kujishughulisha na kitu cho chote isipokuwa chakula alichokula.
Yosefu alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kuvutia; 7baada ya kitambo mke wa Potifa akamtamani Yosefu, akamwambia, “Njoo, ukutane nami kimwili!”
8Lakini Yosefu akakataa. Akamwambia yule mwanamke, “Mimi nikiwa katika uongozi, bwana wangu hahusiki na kitu cho chote katika nyumba hii, kila kitu alicho nacho amenikabidhi. 9Hapa nyumbani hakuna aliye mkuu kuliko mimi. Bwana wangu hakunizuilia kitu cho chote isipokuwa wewe, kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu huu na kutenda dhambi dhidi ya Mungu?” 10Ingawa yule mwanamke aliendelea kumshawishi Yosefu siku baada ya siku, Yosefu alikataa kukutana naye kimwili wala kukaa karibu naye.
11Siku moja Yosefu akaingia ndani ya nyumba kufanya kazi zake, wala hapakuwepo na mfanyakazi ye yote ndani ya nyumba. 12Mke wa Potifa akashika vazi Yosefu alilokuwa amevaa, akamwambia, “Njoo tukutane kimwili!” Lakini Yosefu akaacha vazi lake mkononi mwa huyo mwanamke, akatoka nje ya nyumba akikimbia.
13Yule mwanamke alipoona kwamba Yosefu amemwachia vazi lake mkononi na kukimbilia nje ya nyumba, 14akawaita watumishi wake wa nyumbani, akawaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania ameletwa hapa kutudhihaki! Aliingia hapa ndani ili akutane nami kimwili, lakini nikapiga kelele. 15Aliposikia kelele za kuomba msaada, akaacha vazi lake kando yangu akakimbilia nje.”
16Yule mwanamke akaliweka lile vazi karibu naye mpaka Potifa aliporudi nyumbani. 17Ndipo akamweleza kisa hiki, akisema: “Yule mtumwa wa Kiebrania uliyetuletea alinijia ili kunidhihaki. 18Lakini mara nilipopiga kelele kuomba msaada, akaliacha vazi lake kando yangu akakimbia nje ya nyumba.”
19Potifa aliposikia kisa hiki mkewe alichomweleza, akisema, “Hivi ndivyo mtumwa wako alivyonitenda.” Hasira ya Potifa ikawaka. 20Potifa akamchukua Yosefu na kumweka gerezani, mahali ambapo wahalifu wa mfalme walikuwa wamefungwa.
Lakini wakati Yosefu alipokuwa huko gerezani, 21BWANA alikuwa pamoja naye, akamhurumia na kumpa kibali mbele ya msimamizi wa gereza. 22Kwa hiyo msimamizi wa gereza akamweka Yosefu awe mkuu wa wafungwa pamoja na kusimamia yote ambayo yalitendeka mle gerezani. 23Msimamizi wa gereza hakujishughulisha tena na kitu cho chote kilichokuwa chini ya uangalizi wa Yosefu, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja na Yosefu akimfanikisha kwa kila alichofanya.

Mnyweshaji Na Mwokaji

1Baada ya muda, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, wakamkosea bwana wao, mfalme wa Misri. 2Farao akawakasirikia hawa maafisa wake wawili, mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu, 3akawaweka chini ya ulinzi katika nyumba ya mkuu wa kikosi cha ulinzi katika gereza lile lile alimofungwa Yosefu. 4Mkuu wa kikosi cha ulinzi akawakabidhi kwa Yosefu, naye akawahudumia.
Walipokuwa wamekaa chini ya ulinzi kwa muda, 5kila mmoja wa hao wawili waliokuwa wamewekwa gerezani, yaani mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, waliota ndoto usiku mmoja, na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti.
6Yosefu alipowajia asubuhi yake, akawaona kwamba walikuwa na huzuni. 7Ndipo Yosefu akawauliza maafisa hao wa Farao waliokuwa chini ya ulinzi pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, akasema, “Mbona nyuso zenu zimejaa huzuni leo?”
8Wakamjibu, “Sisi sote tuliota ndoto, lakini hapakuwa na mtu ye yote wa kuzifasiri.”
Ndipo Yosefu akawaambia, “Je, kufasiri ndoto si kazi ya Mungu? Niambieni ndoto zenu.”9Basi mkuu wa wanyweshaji akamweleza Yosefu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, 10nao mzabibu ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua, maua yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu zilizoiva. 11Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, na nikaweka kikombe mkononi mwake.”
12Yosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Matawi matatu ni siku tatu. 13Katika siku hizi tatu, Farao atakutoa gerezani na kukuweka tena kwenye nafasi yako, nawe utaweka kikombe cha Farao mikononi mwake, kama vile ulivyokuwa unafanya ulipokuwa mnyweshaji wake. 14Lakini wakati mambo yatakapokuwia mazuri, unikumbuke, unifanyie wema, useme mema juu yangu kwa Farao ili niondoke huku gerezani. 15Kwa maana nilichukuliwa kwa nguvu kutoka nchi ya Waebrania, na hata hapa nilipo sikufanya lo lote linalostahili niwekwe gerezani.”
16Yule mwokaji mkuu alipoona kuwa Yosefu amefasiri ikiwa na maana nzuri, akamwambia Yosefu, “Mimi pia niliota ndoto: Kichwani mwangu kulikuwepo vikapu vitatu vya mikate. 17Katika kikapu cha juu kulikuwa na aina zote za vyakula vilivyookwa kwa ajili ya Farao, lakini ndege walikuwa wakivila kutoka kwenye kikapu nilichokuwa nimebeba kichwani.”
18Yosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Vikapu vitatu ni siku tatu. 19Katika siku hizi tatu, Farao atakata kichwa chako na kukutundika juu ya mti. Nao ndege watakula nyama ya mwili wako.”
20Mnamo siku ya tatu, ilikuwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Farao, naye akawaandalia maafisa wake wote karamu. Akawatoa gerezani mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu, akawaweka mbele ya maafisa wake: 21Ndipo akamrudisha mnyweshaji kwenye nafasi yake, ili aweke kikombe mikononi mwa Farao tena, 22lakini akamwangika yule mwokaji mkuu, sawasawa na jinsi Yosefu alivyowaambia katika tafsiri yake.
23Pamoja na hayo, mnyweshaji mkuu hakumkumbuka Yosefu, bali alimsahau.

Ndoto Za Farao

1Baada ya miaka miwili kamili kupita, Farao aliota ndoto: Tazama alikuwa amesimama kando ya Mto Nile, 2wakati ng’ombe saba, wazuri na wanono, walitokea mtoni wakajilisha kwenye manyasi. 3Baada yao ng’ombe wengine saba, wabaya na waliokonda, wakatokea mtoni Nile wakasimama kando ya wale wanono ukingoni mwa mto. 4Wale ng’ombe wabaya na waliokonda wakawala wale saba wazuri na wanono. Kisha Farao akaamka.
5Farao akaingia usingizini tena akaota ndoto ya pili: Akaona masuke saba ya nafaka, yenye afya na mazuri, yanakua katika bua moja. 6Baadaye, masuke mengine saba yakachipua, yakiwa membamba yaliyonyaushwa na upepo wa mashariki. 7Masuke yale membamba yakameza yale masuke saba yenye afya na yaliyojaa. Basi Farao akaamka kutoka usingizini, kumbe ilikuwa ndoto.
8Asubuhi yake, alifadhaika akilini, hivyo akawaita waaguzi wote pamoja na watu wenye busara wa Misri. Walipokuja, Farao akawaeleza ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumfasiria.
9Ndipo mnyweshaji mkuu alipomwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kuhusu kosa langu. 10Wakati fulani Farao aliwakasirikia watumishi wake, akanifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa ulinzi. 11Kila mmoja wetu aliota ndoto katika usiku mmoja na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti. 12Basi kijana wa Kiebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, alikuwa mtumishi wa mkuu wa kikosi cha ulinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupa kila mtu tafsiri ya ndoto yake. 13Nayo mambo yakawa sawa kabisa na jinsi alivyotufasiria ndoto zetu: Mimi nilirudishwa kazini mwangu na huyo mtu mwingine akaangikwa.”
14Basi, Farao akatuma Yosefu aitwe, naye akatolewa kifungoni haraka. Baada ya kunyoa na kubadilisha nguo zake akaenda mbele ya Farao.
15Farao akamwambia Yosefu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia ikisemwa kwa habari yako kwamba unapoelezwa ndoto waweza kuifasiri.”
16Yosefu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.”
17Kisha Farao akamwambia Yosefu, “Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa Mto Nile, 18nikawaona ng’ombe saba, wazuri na wanono, wakijitokeza kutoka mtoni wakaja kujilisha kwenye manyasi. 19Baada ya hao, ng’ombe wengine saba wadhaifu wakatokea, wabaya sana na waliokonda. Kamwe sikuwahi kuona ng’ombe wabaya jinsi hiyo katika nchi yote ya Misri. 20Hao ng’ombe waliokonda na wabaya sana wakawala wale ng’ombe saba walionona waliojitokeza kwanza. 21Lakini hata baada ya kuwala, hakuna mtu ambaye angeweza kusema kwamba wamekula, bado walionekana wabaya kama mwanzoni. Kisha nikaamka kutoka usingizini.
22“Pia katika ndoto zangu niliona masuke saba ya nafaka, yamejaa na mazuri, yanakua katika bua moja. 23Baada ya hayo masuke mengine saba yakachipua, yaliyonyauka, membamba na yamekaushwa na upepo wa mashariki. 24Yale masuke membamba ya nafaka yakayameza yale masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka. Nimewaeleza waaguzi, wala hakuna ye yote aliyeweza kunifasiria.”
25Ndipo Yosefu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni ndoto iyo hiyo moja. Mungu amemfunulia Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. 26Ng’ombe saba wazuri ni miaka saba, nayo masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka ni miaka saba, ni ndoto iyo hiyo moja. 27Ng’ombe saba waliokonda na wabaya wale waliojitokeza baadaye ni miaka saba, vivyo hivyo masuke saba ya ngano yaliyodhoofika na kukaushwa na upepo wa mashariki, ni miaka saba ya njaa.
28“Ni kama vile nilivyomwambia Farao: Mungu amemwonyesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. 29Miaka saba ya neema inakuja katika nchi yote ya Misri, 30lakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo neema yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi.
31“Neema iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno. 32Sababu ya ndoto kumjia Farao kwa namna mbili ni kwamba jambo hilo Mungu ameshaamua kwa hakika, naye Mungu atalifanya karibuni.
33“Basi sasa Farao na atafute mtu mwenye akili na hekima ili amweke kuwa msimamizi wa nchi ya Misri. 34Farao na aweke wenye amri nchini kote wakusanye sehemu ya tano ya mavuno ya Misri katika miaka hii saba ya neema. 35Wakusanye chakula chote katika miaka hii saba ya neema inayokuja na kuhifadhi nafaka chini ya mamlaka ya Farao, iwe akiba ya chakula katika miji. 36Chakula hiki kitakuwa akiba ya tahadhari kwa ajili ya nchi, ili kitumike katika ile miaka saba ya njaa itakayokuja Misri, ili nchi isiharibiwe na njaa.”
37Mpango huu ulionekana mzuri kwa Farao na kwa maafisa wake wote. 38Hivyo Farao akawauliza, “Je tunaweza kumpata ye yote kama mtu huyu, ambaye Roho wa Mungu yumo ndani yake?”
39Ndipo Farao akamwambia Yosefu, “Maadamu Mungu amekufunulia yote haya, hakuna mwingine ye yote mwenye akili na hekima kama wewe. 40Wewe utakuwa msimamizi wa jumba langu la kifalme, na watu wangu wote watatii amri zako. Ni kuhusu kiti cha ufalme tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”

Yosefu Msimamizi Wa Misri

41Kwa hiyo Farao akamwambia Yosefu, “Sasa nakuweka uwe msimamizi wa nchi yote ya Misri.” 42Ndipo Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kidoleni mwake na kuivalisha katika kidole cha Yosefu. Akamvika majoho mazuri ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni mwake. 43Akampandisha katika gari lake la farasi kama msaidizi wake, watu wakatangulia wakishangilia, wakisema, “Achieni njia!” Ndivyo Farao alivyomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri.
44Kisha Farao akamwambia Yosefu, “Mimi ni Farao, lakini pasipo neno lako, hakuna mtu mwenye ruhusa kuinua mkono au mguu katika nchi yote ya Misri.” 45Farao akamwita Yosefu Safenath-Panea, pia akampa Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni , kuwa mke wake. Ndipo Yosefu akaitembelea nchi yote ya Misri.
46Yosefu alikuwa na miaka thelathini alipoingia katika utumishi wa Farao mfalme wa Misri. Naye Yosefu akatoka mbele ya Farao akasafiri katika nchi yote ya Misri. 47Katika ile miaka saba ya neema nchi ilizaa mazao kwa wingi sana. 48Yosefu akakusanya chakula chote kilichozalishwa katika ile miaka saba ya neema nchini Misri, akakihifadhi katika ghala za miji. Katika kila mji kulihifadhiwa chakula kilichozalishwa katika mashamba yaliyouzunguka mji huo. 49Yosefu alihifadhi nafaka nyingi, mfano wa mchanga wa bahari, ilikuwa nyingi mno kiasi kwamba walishindwa kuweka kumbukumbu kwa sababu akiba ilizidi sana kupita kipimo.
50Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, alikuwa amemzalia Yosefu wana wawili wa kiume. 51Yosefu akamwita mzaliwa wake wa kwanza Manase, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote pamoja na jamaa yote ya nyumba ya baba yangu.” 52Mwana wa pili akamwita Efraimu, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenistawisha katika nchi ya mateso yangu.”
53Ile miaka saba ya neema huko Misri ikaisha, 54nayo miaka ile saba ya njaa ikaanza, sawasawa na alivyosema Yosefu. Kulikuwa na njaa katika nchi nyingine zote, bali katika nchi yote ya Misri kulikuwa na chakula. 55Wakati nchi yote ya Misri ilipopatwa na njaa, watu wakamlilia Farao ili awape chakula. Ndipo Farao alipowaagiza Wamisri wote, akisema, “Nendeni kwa Yosefu, nanyi mfanye anachowaambia.”
56Wakati njaa ilipokuwa imeenea katika nchi yote, Yosefu akafungua ghala za vyakula na kuwauzia Wamisri nafaka, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno katika nchi yote ya Misri. 57Pia nchi nyingine zote zilikuja Misri kununua nafaka kutoka kwa Yosefu, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno duniani kote.

Ndugu Za Yosefu Waenda Misri

1Wakati Yakobo alipofahamu kuwa kuna nafaka huko Misri, akawaambia wanawe, “Mbona mnakaa tu hapa mnatazamana?” 2Akaendelea kuwaambia, “Nimesikia kuwa huko Misri kuna nafaka. Telemkeni huko mkanunue chakula kwa ajili yetu, ili tuweze kuishi wala tusife.”
3Ndipo wale ndugu kumi wa Yosefu, wakatelemka huko Misri kununua nafaka. 4Lakini Yakobo hakumtuma Benyamini, ndugu yake Yosefu, pamoja na wengine, kwa sababu aliogopa asije akapatwa na madhara. 5Hivyo wana wa Israeli walikuwa miongoni mwa wale waliokwenda Misri kununua nafaka, kwani njaa ilikuwa katika nchi ya Kanaani pia.
6Wakati huo Yosefu alikuwa mtawala wa nchi ya Misri, naye alikuwa ndiye aliyewauzia watu wote nafaka. Kwa hiyo wakati ndugu zake Yosefu walipofika, wakamsujudia hadi nyuso zao zikagusa ardhi. 7Mara Yosefu alipowaona ndugu zake, akawatambua, lakini akajifanya mgeni na kuzungumza nao kwa ukali, akiwauliza, “Ninyi mnatoka wapi?”
Wakamjibu, “Tumetoka katika nchi ya Kanaani kuja kununua chakula.”8Ingawa Yosefu aliwatambua ndugu zake, wao hawakumtambua. 9Ndipo Yosefu alipokumbuka ndoto zake kuwahusu wao, akawaambia, “Ninyi ni wapelelezi! Mmekuja kuangalia mahali ambapo nchi yetu haina ulinzi.”
10Wakamjibu, “Sivyo bwana wangu. Watumishi wako wamekuja kununua chakula. 11Sisi sote ni wana wa baba mmoja. Watumishi wako ni watu waaminifu, wala sio wapelelezi.”
12Akawaambia, “La hasha! Mmekuja kuangalia mahali ambapo nchi yetu haina ulinzi.”
13Lakini wakamjibu, “Watumishi wako walikuwa kumi na wawili, wana wa mtu mmoja ambaye anaishi katika nchi ya Kanaani. Sasa mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu na mwingine alikufa.”
14Yosefu akawaambia, “Ni sawa kabisa kama nilivyowaambia: Ninyi ni wapelelezi! 15Na hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Hakika kama Farao aishivyo, hamtaondoka mahali hapa mpaka ndugu yenu mdogo aje hapa. 16Tumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu, wengine mtawekwa gerezani, ili maneno yenu yajaribiwe kuona kama mnasema kweli. La sivyo, hakika kama Farao aishivyo ninyi ni wapelelezi!” 17Akawaweka wote chini ya ulinzi kwa siku tatu.
18Siku ya tatu Yosefu akawaambia, “Fanyeni hili nanyi mtaishi, kwa maana namwogopa Mungu: 19Ikiwa ninyi ni watu waaminifu, mmoja wa ndugu zenu na abaki kifungoni, nanyi wengine pelekeni nafaka kwa jamaa yenu wanaoteseka kwa njaa. 20Lakini ni lazima mniletee ndugu yenu mdogo hapa, ili maneno yenu yathibitike na kwamba msife.” Wakakubali kufanya hivyo.
21Wakaambiana wao kwa wao, “Hakika tunaadhibiwa kwa sababu ya ndugu yetu. Tuliona jinsi alivyohuzunika alipokuwa anatusihi kuponya maisha yake, lakini hatukumsikiliza, hiyo ndiyo sababu dhiki hii imetupata.”
22Reubeni akawajibu, “Sikuwaambieni msitende dhambi dhidi ya kijana? Lakini hamkunisikiliza! Sasa ni lazima tuadhibiwe kwa ajili ya damu yake.” 23Hawakujua kuwa Yosefu angewaelewa, kwa sababu alitumia mkalimani.
24Yosefu akajitenga nao akaanza kulia, kisha akawarudia na kuzungumza nao tena. Akataka Simeoni akamatwe na kufungwa mbele yao.
25Yosefu akatoa amri ya kujaza magunia yao nafaka na kuweka fedha ya kila mmoja ndani ya gunia lake, kisha wapewe mahitaji ya njiani. Baada ya kufanyiwa hayo yote, 26wakapakiza nafaka juu ya punda zao, wakaondoka.
27Walipofika mahali pa kulala huko njiani mmoja wao akafungua gunia lake ili amlishe punda wake, akakuta fedha yake kwenye mdomo wa gunia lake. 28Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Iko ndani ya gunia langu.”
Mioyo yao ikazimia, na kila mmoja akamgeukia mwenzake wakitetemeka, wakaulizana, “Ni nini hiki Mungu alichotufanyia?”29Walipofika kwa Yakobo baba yao katika nchi ya Kanaani, wakamweleza mambo yote yaliyowapata. Wakasema, 30“Huyo mtu ambaye ndiye bwana katika nchi hiyo alisema nasi kwa ukali, akatutendea kana kwamba sisi tulikuwa tunaipeleleza nchi. 31Lakini tulimwambia, ‘Sisi ni watu waaminifu, sio wapelelezi. 32Tulizaliwa ndugu kumi na wawili, wana wa baba mmoja. Mmoja alikufa, na mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu huko Kanaani.’
33“Ndipo huyo mtu aliye bwana katika nchi hiyo alipotuambia, ‘Hivi ndivyo nitafahamu kuwa ninyi ni watu waaminifu: Mwacheni mmoja wa ndugu zenu pamoja nami hapa, kisha nendeni mpeleke chakula kwa ajili ya jamaa yenu inayoteseka kwa njaa. 34Lakini mleteni huyo ndugu yenu mdogo kwangu, ndipo nitajua kuwa ninyi sio wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Kisha nitamrudisha ndugu yenu, nanyi mtaweza kufanya biashara katika nchi hii.’ ”
35Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka kwenye magunia yao, ndani ya gunia la kila mtu kulikuwa na mfuko wa fedha! Wakati wao na baba yao walipoona mifuko ya fedha, wakaogopa. 36Yakobo baba yao akawaambia, “Ninyi mmenipokonya watoto wangu. Yosefu hayupo na Simeoni hayupo tena na sasa mnataka kumchukua Benyamini. Kila kitu ni kinyume nami!”
37Ndipo Reubeni akamwambia baba yake, “Waweza kuwaua wanangu wote wawili, ikiwa sitamrudisha Benyamini kwako. Mkabidhi Benyamini katika uangalizi wangu, nami nitamrudisha.”
38Lakini Yakobo akasema, “Mwanangu hatashuka huko pamoja nanyi; ndugu yake amekufa naye ndiye peke yake aliyebaki. Ikiwa atapatwa na madhara katika safari mnayoiendea, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini kwa masikitiko.”

Safari Ya Pili Ya Kwenda Misri

1Wakati huu njaa ilikuwa bado ni kali mno katika nchi. 2Hivyo wakati walipokuwa wamemaliza kula nafaka yote waliyoileta kutoka Misri, Yakobo baba yao akawaambia, “Rudini Misri mkatununulie chakula kingine zaidi.”
3Lakini Yuda akamwambia, “Mtu yule alituonya kwa msisitizo, ‘Hamtauona uso wangu tena mpaka mje na ndugu yenu.’ 4Kama utakubali ndugu yetu aende pamoja nasi, tutakwenda kuwanunulia chakula. 5Lakini ikiwa hutamruhusu aende, hatutakwenda, kwa sababu mtu yule alituambia, ‘Hamtauona uso wangu tena mpaka mje pamoja na ndugu yenu.’ ”
6Israeli akauliza, “Kwa nini mkaniletea taabu hii kwa kumwambia yule mtu mlikuwa na ndugu mwingine?”
7Wakamjibu, “Yule mtu alituhoji kwa undani sana habari zetu na za jamaa yetu. Alituuliza, ‘Je, baba yenu bado yungali hai? Je mnaye ndugu mwingine?’ Sisi tulimjibu maswali yake tu. Tungewezaje kujua kwamba angesema, ‘Mleteni mdogo wenu hapa?’ ”
8Ndipo Yuda akamwambia baba yake Israeli, “Mtume kijana pamoja nami, nasi tutaondoka mara, ili sisi na wewe pamoja na watoto wetu tuweze kuishi, wala tusife. 9Mimi mwenyewe nitakuhakikishia usalama wake, mimi mwenyewe nitawajibika kumrudisha. Ikiwa sitamrudisha kwako na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye lawama mbele yako maisha yangu yote. 10Hakika, kama hatukuchelewa kuondoka, tungekuwa tumekwenda na kurudi mara mbili.”
11Basi baba yao Israeli akawaambia, “Kama ni lazima iwe hivyo, basi fanyeni hivi: Wekeni baadhi ya mazao bora ya nchi katika mifuko yenu na mpelekeeni yule mtu kama zawadi, zeri kidogo, asali kidogo, vikolezo, manemane, kungu na lozi. 12Chukueni fedha mara mbili, kwa kuwa mtazirudisha zile fedha zilizowekwa midomoni mwa magunia yenu. Labda ziliwekwa kwa makosa. 13Mchukueni ndugu yenu pia mrudi kwa huyo mtu mara moja. 14Naye Mungu Mwenyezi  awajalieni rehema mbele ya huyo mtu ili apate kumwachia yule ndugu yenu na Benyamini mweze kurudi pamoja. Kwangu mimi kama nikufiwa nimefiwa.”
15Basi hao watu wakazichukua zile zawadi na zile fedha mara mbili pamoja na Benyamini. Wakafanya haraka kwenda Misri na walipofika wakajionyesha kwa Yosefu. 16Yosefu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wachukue watu hawa nyumbani kwangu, mchinje mnyama na kuandalia chakula kwa kuwa watakula chakula cha mchana pamoja nami.”
17Yule Msimamizi akafanya kama Yosefu alivyomwambia na akawachukua wale watu nyumbani kwa Yosefu. 18Basi watu hao wakaogopa walipopelekwa nyumbani kwa Yosefu. Wakafikiri, “Tumeletwa hapa kwa ajili ya zile fedha zilizorudishwa katika magunia yetu mara ile ya kwanza. Anataka kutushambulia na kutushinda, atuchukue sisi kama watumwa, na atwae hawa punda zetu.”
19Hivyo wakamwendea msimamizi wa nyumba wa Yosefu na kuzungumza naye kwenye ingilio la nyumbani. 20Wakasema, “Tafadhali bwana, tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula. 21Lakini mahali pale tulipotua wakati wa jioni tulifungua magunia yetu, na kila mmoja wetu akakuta fedha zake, kwenye mdomo wa gunia lake kiasi kile kile tulicholeta. Kwa hiyo tumezirudisha. 22Pia tumeleta fedha nyingine kwa ajili ya kununulia chakula. Hatujui ni nani aliziweka fedha hizo katika magunia yetu.”
23Akawaambia, “Vema msiogope. Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, amewapa ninyi hazina katika magunia yenu; mimi nilipokea fedha yenu.” Ndipo akawaletea Simeoni.
24Msimamizi akawapeleka wale watu katika nyumba ya Yosefu, akawapa maji ya kunawa miguu na kuwapa punda wao majani. 25Wakaandaa zawadi zao ili wampe Yosefu wakati atakapofika adhuhuri, kwa kuwa walikuwa wamesikia kwamba watakula chakula huko.
26Yosefu alipokuja nyumbani, walimkabidhi zile zawadi walizokuwa nazo, ambazo walikuwa wamezileta mle nyumbani, nao wakamsujudia hadi nchi. 27Akawauliza kuhusu hali yao, kisha akawaambia, “Yule baba yenu mzee mliyeniambia habari zake, yu hali gani? Je, bado yu hai?”
28Wakamjibu, “Mtumishi wako baba yetu bado anaishi na ni mzima.” Kisha wakainama chini kumpa heshima.
29Alipotazama na kumwona Benyamini ndugu yake, mwana wa mama yake hasa, akauliza, “Je, huyu ndiye ndugu yenu wa mwisho, ambaye mlinieleza habari zake?” Ndipo akasema, “Mungu na akufadhili, mwanangu.” 30Akiwa ameguswa sana kwa kumwona ndugu yake, Yosefu akatoka nje kwa haraka na kutafuta mahali pa kulilia. Akaingia kwenye chumba chake cha pekee na kulilia humo.
31Baada ya kunawa uso wake, akatoka nje na huku akijizuia akasema, “Pakueni chakula.”
32Wakampakulia Yosefu peke yake, ndugu zake peke yao na Wamisri waliokula pamoja naye peke yao, kwa sababu Wamisri wasingeweza kula pamoja na Waebrania, kwa maana ilikuwa ni chukizo kwa Wamisri. 33Watu hao walikuwa wameketi mbele yake kwa mfuatano wa umri wao, kuanzia mzaliwa wa kwanza hadi mzaliwa wa mwisho, wakatazamana wao kwa wao kwa mshangao. 34Wakati walipopelekewa sehemu ya chakula kutoka mezani mwa Yosefu, sehemu ya Benyamini ilikuwa mara tano zaidi ya sehemu ya wale wengine. Kwa hiyo wakanywa na kufurahi pamoja naye.

Kikombe Cha Fedha Ndani Ya Gunia

1Kisha Yosefu akampa yule msimamizi wa nyumbani mwake maagizo haya: “Jaza magunia ya watu hawa kiasi cha chakula ambacho wanaweza kuchukua, na uweke fedha ya kila mtu kwenye mdomo wa gunia lake. 2Kisha weka kikombe changu kile cha fedha kwenye mdomo wa gunia la yule mdogo wa wote pamoja na fedha zake ambazo angenunulia nafaka yake.” Naye akafanya kama Yosefu alivyosema.
3Kulipopambazuka, hao watu wakaruhusiwa kuondoka pamoja na punda zao. 4Kabla hawajafika mbali kutoka mjini, Yosefu akamwambia mtumishi wake, “Wafuatilie wale watu mara moja, utakapowakuta, waambie, ‘Kwa nini mmelipiza wema kwa ubaya? 5Je, kikombe hiki sicho anachonywea bwana wangu na pia hukitumia kwa kutabiri mambo yajayo? Hili ni jambo ovu mlilolitenda.’ ”
6Alipowafikia, akarudia maneno haya kwao. 7Lakini wakamwambia mtumishi, “Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? Liwe mbali na watumishi wako wasije wakafanya jambo kama hilo! 8Hata hivyo tulikurudishia zile fedha kutoka nchi ya Kanaani ambazo tulizikuta kwenye midomo ya magunia yetu. Hivyo kwa nini tuibe fedha au dhahabu kutoka nyumbani kwa bwana wako? 9Ikiwa ye yote miongoni mwa watumishi wako atapatikana nacho, auawe, na sisi wengine tutakuwa watumwa wa bwana wangu.”
10Akajibu, “Vema sana; na iwe kama msemavyo. Ye yote atakayekutwa nacho atakuwa mtumwa wangu, lakini ninyi wengine mtakuwa hamna lawama.”
11Kila mmoja wao akafanya haraka kushusha gunia lake chini na kulifungua. 12Ndipo msimamizi akaendelea kutafuta, akianzia kwa mkubwa wa wote na akaishia kwa mdogo wa wote. Basi kikombe kikapatikana katika gunia la Benyamini. 13Kwa jambo hili, wakararua nguo zao. Ndipo wote wakapakiza mizigo yao juu ya punda zao na kurudi mjini.
14Yosefu alikuwa bado yuko nyumbani mwake wakati Yuda na kaka zake walipoingia, wote wakajitupa chini mbele yake. 15Yosefu akawaambia, “Ni jambo gani hili mlilolifanya? Hamjui kuwa mtu kama mimi anaweza kufahamu mambo kwa njia ya kutabiri?”
16Yuda akajibu, “Tutaweza kusema nini kwa bwana wangu? Tutaweza kuzungumza nini? Tutawezaje kuthibitisha kwamba hatuna hatia? Mungu amefunua hatia ya watumishi wako. Sasa sisi tu watumwa wa bwana wangu, sisi wenyewe pamoja na yule aliyepatikana na kikombe.”
17Lakini Yosefu alisema, “Liwe mbali nami kufanya jambo kama hili! Mtu yule tu aliyekutwa na kikombe ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Ninyi wengine, rudini kwa baba yenu kwa amani.”
18Ndipo Yuda akamwendea na kumwambia: “Tafadhali bwana wangu, mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa bwana wangu. Usimkasirikie mtumishi wako, ingawa wewe ni sawa na Farao mwenyewe. 19Bwana wangu aliwauliza watumishi wake, ‘Mnaye baba au ndugu?’ 20Nasi tukakujibu, ‘Tunaye baba yetu ambaye ni mzee; pia yupo mwanawe mdogo aliyezaliwa katika uzee wake. Ndugu yake amekufa, na huyu mdogo ndiye mwana pekee kwa mama yake aliyebaki, naye baba yake anampenda.’ ”
21“Ndipo ulipowaambia watumishi wako, ‘Mleteni kwangu ili niweze kumwona kwa macho yangu mwenyewe.’ 22Nasi tukamwambia bwana wangu, ‘Kijana hawezi kumwacha baba yake; akimwacha, baba yake atakufa.’ 23Lakini ukawaambia watumishi wako, ‘Ndugu yenu mdogo asiposhuka pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena.’ 24Tuliporudi nyumbani kwa mtumwa wako baba yangu, tulimwambia lile bwana wangu alilokuwa amesema.
25“Ndipo baba yetu aliposema, ‘Rudini Misri mkanunue chakula kingine.’ 26Lakini tukamwambia, ‘Hatuwezi kushuka Misri mpaka ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi ndipo tutakapokwenda. Hatutaweza kuuona uso wa yule mtu mpaka ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi.’
27“Mtumwa wako baba yangu alituambia, ‘Mnajua mke wangu alinizalia wana wawili. 28Mmojawapo alipotea, nami nikasema, “Hakika ameraruliwa vipande vipande.” Nami sijamwona tangu wakati huo. 29Ikiwa mtaniondolea huyu tena na akapatwa na madhara, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini nikiwa mwenye huzuni.’
30“Hivyo sasa, kama kijana hatakuwa pamoja nasi nitakaporudi kwa mtumishi wako baba yangu, na kama baba yangu, ambaye maisha yake yamefungamanishwa na uhai wa kijana huyu, 31akiona kijana hayupo nasi, atakufa. Watumishi wako watashusha kichwa chenye mvi cha baba yetu kaburini kwa huzuni. 32Mtumwa wako alimhakikishia baba yangu usalama wa kijana. Nikamwambia, ‘Kama sikumrudisha kwako nitakuwa mwenye lawama mbele yako, baba yangu, maisha yangu yote!’
33“Sasa basi, tafadhali mruhusu mtumishi abaki hapa kama mtumwa wa bwana wangu badala ya kijana, naye kijana umruhusu arudi na ndugu zake. 34Ninawezaje kurudi kwa baba yangu kama kijana hatakuwa pamoja nami? La hasha! Usiniache nikaone huzuni ile itakayompata baba yangu.”

Yosefu Anajitambulisha

1Hapo Yosefu hakuweza kujizuia zaidi mbele ya wote waliokuwa wamesimama karibu naye, akapaza sauti, akasema, “Mwondoeni kila mtu mbele yangu!” Kwa hiyo hapakuwepo mtu ye yote pamoja na Yosefu alipojitambulisha kwa ndugu zake. 2Naye akalia kwa sauti kubwa kiasi kwamba Wamisri walimsikia, hata watu wa nyumbani mwa Farao wakapata hizo habari.
3Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu! Je, baba yangu angali hai bado?” Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwa sababu walipatwa na hofu kuu mbele yake.
4Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yosefu, yule ambaye mlimwuza Misri! 5Sasa, msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi. 6Kwa miaka miwili sasa imekuwepo njaa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwepo kulima wala kuvuna. 7Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuhifadhi mabaki kwa ajili yenu katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu.
8“Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kuwa baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote. 9Sasa rudini haraka kwa baba yangu na mwambieni, ‘Hili ndilo mwanao Yosefu asemalo: Mungu amenifanya mimi kuwa bwana wa Misri yote. Shuka uje kwangu, wala usikawie. 10Nawe utaishi katika nchi ya Gosheni na kuwa karibu nami, wewe, watoto wako na wajukuu wako, makundi yako ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, pamoja na vyote ulivyo navyo. 11Nitawatunza huko, kwa sababu bado iko miaka mingine mitano inayokuja ya njaa. La sivyo, wewe na nyumba yako na wote ulionao mtakuwa fukara.’
12“Mnaweza kujionea wenyewe, hata ndugu yangu Benyamini, kwamba hakika ni mimi ninayezungumza nanyi. 13Mwambieni baba yangu juu ya heshima yote niliyopewa huku Misri, na kuhusu kila kitu mlichokiona. Mleteni baba yangu huku haraka.”
14Ndipo akamkumbatia Benyamini ndugu yake na kulia, naye Benyamini akamkumbatia akilia. 15Pia akawabusu ndugu zake wote, huku akilia. Baada ya hayo ndugu zake wakazungumza naye.
16Habari zilipofika kwenye jumba la kifalme la Farao kwamba ndugu zake Yosefu wamefika, Farao na maafisa wake wote wakafurahi. 17Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako, ‘Fanyeni hivi: Pakieni wanyama wenu mrudi mpaka nchi ya Kanaani, 18mkamlete baba yenu na jamaa zenu kwangu. Nitawapa sehemu nzuri sana ya nchi ya Misri nanyi mtafurahia unono wa nchi.’
19“Mnaagizwa pia kuwaambia, ‘Fanyeni hivi: Chukueni magari ya kukokotwa kutoka Misri, kwa ajili ya watoto wenu na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. 20Msijali kamwe kuhusu mali zenu, kwa sababu mema yote ya Misri yatakuwa yenu.’ ”
21Hivyo wana wa Israeli wakafanya hivyo. Yosefu akawapa magari ya kukokotwa, kama Farao alivyoagiza, pia akawapa mahitaji kwa ajili ya safari yao. 22Kila mmoja mavazi mapya, lakini Benyamini akampa shekeli 300  za fedha, na jozi tano za nguo. 23Hivi ndivyo vitu alivyotuma kwa baba yake: punda kumi waliochukua vitu vizuri vya Misri, punda wake kumi waliobeba nafaka, mikate na mahitaji mengine ya safari. 24Akaagana na ndugu zake walipokuwa wakiondoka, akawaambia, “Msigombane njiani!”
25Basi wakatoka Misri na kufika kwa baba yao Yakobo katika nchi ya Kanaani. 26Wakamwambia baba yao, “Yosefu angali hai! Ukweli ni kwamba yeye ndiye mtawala wa Misri yote.” Yakobo akapigwa na bumbuwazi; hakuwasadiki. 27Lakini walipokwisha kumweleza kila kitu ambacho Yosefu alikuwa amewaambia, na alipoona magari ya kukokotwa Yosefu aliyokuwa amempelekea ya kumchukua aende Misri, roho ya baba yao Yakobo ikahuishwa. 28Ndipo Israeli akasema, “Nimesadiki! Mwanangu Yosefu bado yu hai. Nitakwenda nikamwone kabla sijafa.”

Yakobo Aenda Misri

1Hivyo Israeli akaondoka na vyote vilivyokuwa mali yake, naye alipofika Beer-Sheba, akamtolea dhabihu Mungu wa Isaki baba yake.
2Mungu akanena na Israeli katika maono usiku na kusema, “Yakobo! Yakobo!”
Akajibu, “Mimi hapa.”3Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako, usiogope kushuka Misri, kwa maana huko nitakufanya taifa kubwa. 4Nitashuka Misri pamoja nawe, nami hakika nitakurudisha tena Kanaani. Mikono ya Yosefu mwenyewe ndiyo itakayofunga macho yako.”
5Ndipo Yakobo akaondoka Beer-Sheba nao wana wa Israeli wakamchukua baba yao Yakobo na watoto wao na wake zao katika magari ya kukokotwa yale Farao aliyokuwa amempelekea kumsafirisha. 6Wakachukua pia mifugo yao na mali walizokuwa wamezipata Kanaani, Yakobo na uzao wake wote wakashuka Misri. 7Akawachukua wanawe na binti zake, wajukuu wake wa kiume na wa kike, yaani uzao wake wote mpaka Misri.
8Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli (Yakobo na wazao wake), waliokwenda Misri:

  • Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo.

9Wana wa Reubeni ni: Hanoki, Palu, Hesroni na Karmi. 10Wana wa Simeoni ni: Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani. 11Wana wa Lawi ni: Gershoni, Kohathi na Merari. 12Wana wa Yuda ni: Eri, Onani, Shela, Peresi na Zera (lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani). Wana wa Peresi ni: Hesroni na Hamuli. 13Wana wa Isakari ni: Tola, Puva, Yashubu na Shimroni. 14Wana wa Zabuloni ni: Seredi, Eloni na Yaleeli.15Hawa ndio wana wa Lea aliomzalia Yakobo huko Padan-Aramu pamoja na binti yake Dina. Jumla ya wanawe na binti zake walikuwa thelathini na watatu. 16

  • Wana wa Gadi ni:
  • Sefoni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi na Areli.

17Wana wa Asheri ni: Imna, Ishva, Ishvi na Beria. Dada yao alikuwa Sera. Wana wa Beria ni: Heberi na Malkieli.18Hawa ndio watoto Zilpa aliomzalia Yakobo, ambao Labani alimpa binti yake Lea; jumla yao walikuwa kumi na sita. 19

  • Wana wa Raheli mke wa Yakobo ni:
  • Yosefu na Benyamini.

20Huko Misri, Asenathi binti wa Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni 46:20 Yaani Heliopoli (Mji wa Jua) , alimzalia Yosefu wana wawili, Manase na Efraimu. 21Wana wa Benyamini ni: Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu na Ardi.22Hawa ndio wana wa Raheli aliomzalia Yakobo; jumla yao ni kumi na wanne. 23

  • Mwana wa Dani ni:
  • Hushimu.

24Wana wa Naftali ni: Yasieli, Guni, Yeseri na Shilemu.25Hawa walikuwa wana wa Bilha aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alikuwa amempa Raheli binti yake; jumla yao walikuwa saba.
26Wote waliokwenda Misri pamoja na Yakobo, ambao walikuwa wazao wake hasa pasipo kuhesabu wakwe zake, walikuwa watu sitini na sita. 27Pamoja na wana wawili waliozaliwa na Yosefu huko Misri, jumla yote ya jamaa ya Yakobo, waliokwenda Misri, walikuwa sabini.
28Basi Yakobo akamtanguliza Yuda aende kwa Yosefu ili amwelekeze njia ya Gosheni. Walipofika nchi ya Gosheni, 29gari kubwa zuri la Yosefu liliandaliwa, naye akaenda Gosheni kumlaki baba yake Israeli. Mara Yosefu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu.
30Israeli akamwambia Yosefu, “Sasa niko tayari kufa, kwa kuwa nimejionea mwenyewe kwamba bado uko hai.”
31Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, “Nitapanda kwa Farao na kumwambia, ‘Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa baba yangu, ambao walikuwa wakiishi katika nchi ya Kanaani, wamekuja kwangu. 32Watu hao ni wachunga mifugo, huchunga mifugo, wamekuja na makundi ya kondoo, mbuzi na ng’ombe pamoja na kila kitu walichonacho.’ 33Farao atakapowaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’ 34Mjibuni, ‘Watumwa wako wamekuwa wachunga mifugo tangu ujana wetu mpaka sasa, kama baba zetu walivyofanya.’ Ndipo mtakaporuhusiwa kukaa katika nchi ya Gosheni, kwa kuwa wachunga mifugo wote ni chukizo kwa Wamisri.”

Yakobo Ambariki Farao

1Yosefu akaenda na kumwambia Farao, “Baba yangu na ndugu zangu wamekuja kutoka nchi ya Kanaani wakiwa na makundi yao ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, pamoja na kila kitu walichonacho, nao sasa wapo huko Gosheni.” 2Akachagua ndugu zake watano na kuwaonyesha kwa Farao.
3Farao akawauliza hao ndugu zake, “Kazi yenu ni nini?”
Wakamjibu, “Watumishi wako ni wachunga mifugo, kama vile baba zetu walivyokuwa.” 4Pia wakamwambia, “Tumekuja kukaa huku kwa muda mfupi, kwa sababu njaa ni kali huko Kanaani, na mifugo ya watumishi wako haina malisho. Kwa hiyo sasa, tafadhali uruhusu watumishi wako wakae huko Gosheni.”
5Farao akamwambia Yosefu, “Baba yako na ndugu zako wamekuja kwako, 6nayo nchi ya Misri ipo mbele yako, uwakalishe baba yako na ndugu zako katika sehemu iliyo bora kupita zote katika nchi. Na waishi Gosheni. Kama unamfahamu ye yote miongoni mwao mwenye uwezo maalum, waweke wawe wasimamizi wa mifugo yangu.”
7Ndipo Yosefu akamleta Yakobo baba yake na kumtambulisha mbele ya Farao. Baada ya Yakobo kumbariki Farao, 8Farao akamwuliza, “Je una umri gani?”
9Naye Yakobo akamwambia Farao, “Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni miaka 130. Miaka yangu imekuwa michache na ya taabu, wala haikufikia miaka ya kusafiri ya baba zangu.” 10Kisha Yakobo akambariki Farao, naye akaondoka mbele ya uso wake.
11Ndipo Yosefu akawakalisha baba yake na ndugu zake katika nchi ya Misri na kuwapa milki katika sehemu bora sana ya nchi, wilaya ya Ramesesi, kama Farao alivyoelekeza. 12Pia Yosefu akampa baba yake, na ndugu zake na wote wa nyumbani mwa baba yake vyakula, kwa kulingana na hesabu ya watoto wao.

Uongozi Wa Yosefu Wakati Wa Njaa

13Hata hivyo, hapakuwepo chakula katika sehemu yote kwa kuwa njaa ilikuwa kali sana; Misri na Kanaani zote zikaharibiwa kwa sababu ya njaa. 14Yosefu akakusanya fedha zote zilizopatikana kutoka katika mauzo ya nafaka huko Misri na Kanaani, akazileta kwenye jumba la kifalme la Farao. 15Fedha za watu wa Misri na Kanaani zilipokwisha, Wamisri wote wakamjia Yosefu na kumwambia, “Tupatie chakula. Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Fedha zetu zimekwisha.”
16Yosefu akawaambia, “Basi leteni mifugo yenu, nitawauzia chakula kwa kubadilisha na mifugo yenu, kwa kuwa fedha zenu zimekwisha.” 17Kwa hiyo wakaleta mifugo yao kwa Yosefu, naye akawapa chakula kwa kubadilishana na farasi zao, kondoo na mbuzi zao, ng’ombe na punda zao. Katika mwaka huo wote Yosefu akawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote.
18Mwaka ule ulipokwisha, wakamjia mwaka uliofuata na kumwambia, “Hatuwezi kuficha ukweli mbele za bwana wetu kwamba, kwa kuwa fedha zetu zimekwisha na wanyama wetu ni mali yako, sasa hakuna cho chote kilichosalia kwa ajili ya bwana wetu isipokuwa miili yetu na ardhi yetu. 19Kwa nini tuangamie mbele ya macho yako, sisi pamoja na nchi yetu? Utununue sisi pamoja na ardhi yetu ili kubadilishana kwa chakula. Nasi pamoja na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao. Tupe sisi mbegu ili tuweze kuishi wala tusife, nchi yetu isije ikawa ukiwa.”
20Kwa hiyo Yosefu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri. Wamisri, mmoja baada ya mwingine, waliuza mashamba yao, kwa sababu njaa ilikuwa kali sana kwao. Nchi ikawa mali ya Farao, 21naye Yosefu akawafanya watu watumike kama watumwa, kuanzia upande mmoja wa Misri hadi upande mwingine. 22Hata hivyo, hakununua nchi ya makuhani, kwa sababu walikuwa wanapata mgawo wao wa kawaida kutoka kwa Farao, nao walikuwa na chakula cha kuwatosha kutokana na mgawo waliopewa na Farao. Hii ndiyo sababu hawakuuza ardhi yao.
23Yosefu akawaambia watu, “Kwa vile nimewanunua ninyi pamoja na nchi yenu leo kuwa mali ya Farao, hapa kuna mbegu kwa ajili yenu ili mweze kuziotesha. 24Lakini wakati mazao yatakapokuwa tayari, mpeni Farao sehemu ya tano. Sehemu hizo nne zitakazobaki mtaziweka kama mbegu kwa ajili ya mashamba na kwa ajili ya chakula chenu wenyewe na cha watu wa nyumbani mwenu na watoto wenu.”
25Wakamwambia, “Umeokoa maisha yetu. Basi na tupate kibali mbele ya macho ya bwana wetu; tutakuwa watumwa wa Farao.”
26Basi Yosefu akaiweka iwe sheria kuhusu nchi ya Misri, ambayo inatumika mpaka leo, kwamba, sehemu ya tano ya mazao ni mali ya Farao. Ni nchi ya makuhani tu ambayo haikuwa ya Farao.
27Basi Waisraeli wakaishi Misri katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali huko wakastawi na kuongezeka kwa wingi sana.
28Yakobo akaishi Misri miaka kumi na saba, nayo miaka ya maisha yake ilikuwa 147. 29Wakati ulipokaribia wa Israeli kufa, akamwita mwanawe Yosefu na kumwambia, “Kama nimepata kibali machoni pake, weka mkono wako chini ya paja langu na uniahidi kuwa utanifanyia fadhili na uaminifu. Usinizike Misri, 30lakini nitakapopumzika na baba zangu, unichukue kutoka Misri, ukanizike walipozikwa.”
Yosefu akamwambia, “Nitafanya kama unavyosema.”31Akamwambia, “Niapie.” Ndipo Yosefu akamwapia, naye Israeli akaabudu, akijiegemeza kwenye mchago wa kitanda chake.