Skip to content

Mwanzo 1-2

Siku Sita Za Uumbaji Na Sabato

1Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. 2Wakati huu Dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu, giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametanda juu ya maji. 3

  • Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo.

4Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. 5Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza. 6Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.” 7Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi na akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. 8Mungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili. 9Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. 10Mungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema. 11Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. 12Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema. 13Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu. 14

  • Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe mchana na usiku, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka,

15nayo iwe ndiyo mianga kwenye nafasi ya anga itoe nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. 16Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. 17Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia, 18itawale mchana na usiku, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 19Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne. 20Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” 21Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini, kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 22Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mkaongezeke mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.” 23Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano. 24Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo. 25Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wafugwao kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 26Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.” 27

Kwa hiyo Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,
kwa mfano wa Mungu alimuumba;
mwanaume na mwanamke aliwaumba.

28Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”
29Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa kwa ajili ya chakula chenu, 30cha wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi. Kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.
31Mungu akatazama vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.

1Kwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo. 2

  • Katika siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya, hivyo siku ya saba akapumzika kutoka kazi zake zote.

3Mungu akaibariki siku ya saba akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kazi zote za kuumba alizokuwa amefanya. Adamu Na Eva 4Haya ndiyo maelezo ya mbingu na dunia wakati zilipoumbwa.
BWANA Mungu alipoziumba mbingu na dunia,
 5hapakuwepo na mche wa shambani uliokuwa umejitokeza ardhini, wala hapakuwepo na mmea wa shamba uliokuwa umeota, kwa kuwa BWANA Mungu alikuwa hajanyeshea mvua juu ya nchi, na hapakuwepo mtu wa kuilima ardhi, 6lakini umande ulitokeza kutoka ardhini na kunyesha uso wote wa nchi: 7BWANA Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi  ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, mtu akawa kiumbe hai.
8Basi BWANA Mungu alikuwa ameotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni, huko akamweka huyo mtu aliyemuumba. 9BWANA Mungu akafanya aina zote za miti ziote kutoka ardhini, miti yenye kupendeza macho na mizuri kwa chakula. Katikati ya bustani ulikuwepo mti wa uzima na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.
10Mto wa kunyeshea bustani ulitiririka toka Edeni, kuanzia hapa ukagawanyika kuwa mito minne. 11Mto wa kwanza uliitwa Pishoni, nao huzunguka nchi yote ya Havila ambako kuna dhahabu. 12(Dhahabu ya nchi hiyo ni nzuri, lulu na vito shohamu pia hupatikana huko.) 13Jina la mto wa pili ni Gihoni, ambao huzunguka nchi yote ya Kushi. 14Jina la mto wa tatu ni Tigrisi, unaopita mashariki ya Ashuru. Mto wa nne ni Eufrati.
15BWANA Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza. 16BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akamwambia, “Uko huru kula matunda ya mti wo wote katika bustani, 17lakini kamwe usile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa.”
18BWANA Mungu akasema, “Si vyema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.”
19Basi BWANA Mungu alikuwa amefanyiza kutoka katika ardhi wanyama wote wa porini na ndege wote wa angani. Akawaleta kwa huyu mtu aone atawaitaje, nalo jina lo lote alilokiita kila kiumbe hai, likawa ndilo jina lake. 20Hivyo Adamu akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, ndege wa angani, na wanyama wote wa porini.
Lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi wa kumfaa.
 21Hivyo BWANA Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama. 22Kisha BWANA Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanaume.
23Huyo mwanaume akasema,“Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu
na nyama ya nyama yangu,
ataitwa ‘mwanamke ,’
kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.”

24Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
25Adamu na mkewe wote wawili walikuwa uchi, wala hawakuona aibu.