Skip to content

Yohana 13-16

Yesu Awanawisha Wanafunzi Wake Miguu

1Ilikuwa mara tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua ya kuwa wakati wake wa kuondoka ulimwenguni ili kurudi kwa Baba umewadia. Alikuwa amewapenda watu wake waliokuwa ulimwenguni, naam, aliwapenda hadi kipimo cha mwisho.
2Wakati alipokuwa akila chakula cha jioni na wanafunzi wake, ibilisi alikuwa amekwisha kutia ndani ya moyo wa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni, wazo la kumsaliti Yesu. 3Yesu akijua ya kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, 4hivyo aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni. 5Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni.
6Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?”
7Yesu akamjibu, “Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa.”
8Petro akamwambia, “La, wewe hutaninawisha miguu kamwe.”
Yesu akamjibu, “Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami.”
9Ndipo Simoni Petro akajibu, “Usininawishe miguu peke yake, bali pamoja na mikono na kichwa pia!”
10Yesu akamjibu, “Mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake wote ni safi. Ninyi ni safi, ingawa si kila mmoja wenu.” 11Kwa kuwa yeye alijua ni nani ambaye angemsaliti, ndiyo sababu akasema si kila mmoja aliyekuwa safi.
12Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi, akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia? 13Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana,’ hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. 14Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. 15Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. 16Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala anayetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. 17Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri yenu ninyi kama mkiyatenda.
18“Sisemi kuhusu ninyi nyote. Ninawajua wale niliowachagua. Lakini ni ili maandiko yapate kutimia, ‘Yeye aliyekula chakula changu, ameinua kisigino chake dhidi yangu.’
19“Ninawaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa Mimi ndiye. 20Amin, amin, nawaambia, ye yote anayempokea yule niliyemtuma, anipokea mimi, naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma mimi.”

Yesu Anatabiri Kusalitiwa Kwake

21Baada ya kusema haya, Yesu alifadhaika sana moyoni, akasema, “Amin, amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”
22Wanafunzi wake wakatazamana bila kujua kuwa alikuwa anamsema nani. 23Mmoja wa wanafunzi wake, ambaye Yesu alimpenda sana alikuwa ameegama kifuani mwa Yesu. 24Simoni Petro akampungia mkono yule mwanafunzi akamwambia, “Mwulize anamaanisha ni nani.”
25Yule mwanafunzi akiwa amemwegemea Yesu akamwuliza, “Bwana tuambie ni nani?”
26Yesu akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya kwenye bakuli.” Hivyo baada ya kukichovya kile kipande cha mkate, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. 27Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia.
Yesu akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda litende haraka.”
 28Hakuna hata mmoja wa wale waliokuwa ameketi nao chakulani aliyeelewa kwa nini Yesu alimwambia hivyo. 29Kwa kuwa Yuda alikuwa mtunza fedha, wengine walifikiri Yesu alikuwa amemwambia akanunue vitu vilivyohitajika kwa ajili ya Sikukuu, au kuwapa maskini cho chote. 30Mara tu baada ya kupokea ule mkate, Yuda akatoka nje. Wakati huo ulikuwa ni usiku.

Yesu Atabiri Petro Kumkana

31Baada ya Yuda kutoka nje, Yesu akasema, “Sasa Mwana wa Adamu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. 32Ikiwa Mungu ametukuzwa ndani ya Mwana, Mungu atamtukuza Mwana ndani yake mwenyewe naye atamtukuza mara.
33“Watoto wangu, mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo. Mtanitafuta na kama vile nilivyowaambia Wayahudi, vivyo hivyo sasa nawaambia na ninyi. Niendako, ninyi hamwezi kuja.
34“Amri mpya nawapa: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi, vivyo hivyo nanyi mpendane. 35Kama mkipendana ninyi kwa ninyi, kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu”
36Simoni Petro akamwuliza, “Bwana, unakwenda wapi?”
Yesu akamjibu, “Ninakokwenda huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye.”
37Petro akamwuliza tena, “Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Mimi niko tayari kuutoa uhai wangu kwa ajili yako.”
38Yesu akamjibu, “Je, ni kweli uko tayari kuutoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin nakuambia, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

Yesu Awatia Moyo Wanafunzi Wake

1Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Nakwenda kuwaandalia makao. 3Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. 4Ninyi mnajua njia ya kufika ninakokwenda.”

Yesu Ndiye Njia Ya Kwenda Kwa Baba

5Tomasi akamwam bia, “Bwana, sisi hatujui unakokwenda, tutaijuaje njia?”
6Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu. 7Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa, mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.”
8Filipo akamwambia, “Bwana, tuonyeshe Baba yako yatosha.”
9Yesu akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu ye yote aliyeniona mimi, amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuonyeshe Baba?’ 10Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi. 11Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yangu, la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo. 12Amin, amin nawaambia, ye yote aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo yeye atazifanya, naam na kubwa kuliko hizi atazifanya, kwa sababu mimi ninakwenda kwa Baba. 13Nanyi mkiomba lo lote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana. 14Kama mkiniomba lo lote kwa Jina langu nitalifanya.

Yesu Aahidi Roho Mtakatifu

15“Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. 16Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. 17Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu. 18Sitawaacha ninyi yatima, naja kwenu. 19Bado kitambo kidogo ulimwengu hautaniona tena, ila ninyi mtaniona, kwa kuwa mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. 20Wakati huo mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba na ninyi mko ndani yangu na mimi niko ndani yenu. 21Ye yote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye, naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.”
22Ndipo Yuda, siyo Iskariote, akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?”
23Yesu akamjibu, “Mtu ye yote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. 24Mtu ye yote asiyenipenda hayashiki maneno yangu na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma.
25“Nimewaambia mambo haya yote wakati nikiwa bado niko pamoja nanyi. 26Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.
28“Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa nakwenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuliko mimi. 29Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini. 30Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu, 31lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile vile kama Baba alivyoniamuru.
“Haya inukeni; twendeni zetu.

Yesu Mzabibu Wa Kweli

1“Mimi ndimi mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima. 2Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi lizaalo, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. 3Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi. 4Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda.
5“Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lo lote. 6Mtu ye yote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi kama hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. 7Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lo lote mtakalo, nanyi mtatendewa. 8Kwa hiyo Baba yangu hutukuzwa, kwa vile mzaavyo matunda mengi, nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.
9“Kama vile Baba alivyonipenda mimi, hivyo ndivyo mimi nilivyowapenda ninyi. Basi kaeni katika pendo langu. 10Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. 11Nimewaambia mambo haya ili furaha yangu iwe ndani yenu na furaha yenu iwe kamili. 12Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi. 13Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. 14Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu. 16Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda na matunda yenu yapate kudumu, ili lo lote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape. 17Amri yangu ndiyo hii: Mpendane.

Ulimwengu Wawachukia Wanafunzi

18“Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba ulinichukia mimi kabla yenu. 19Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungeliwapenda kama vile unavyowapenda walio wake. Kwa sababu ninyi si wa ulimwengu, lakini mimi nimewachagua kutoka katika ulimwengu, hii ndiyo sababu ulimwengu unawachukia. 20Kumbukeni lile neno nililowaambia, ‘Hakuna mtumishi aliye mkuu kuliko bwana wake.’ Kama wamenitesa mimi, nanyi pia watawatesa, kama wamelishika neno langu, watalishika na neno lenu pia. 21Watawatendea ninyi haya yote kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma. 22Kama sikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa hawana udhuru kwa ajili ya dhambi zao. 23Ye yote anayenichukia mimi, anamchukia pia na Baba yangu. 24Kama sikuwa nimefanya miujiza ambayo haijapata kufanywa na mtu mwingine ye yote, wasingalikuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa wameiona miujiza hii na bado wakatuchukia mimi na Baba yangu. 25Lakini hii ni kutimiza lile neno lililoandikwa kwenye Torati kwamba ‘Walinichukia pasipo sababu.’
26“Lakini atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, yaani, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. 27Ninyi nanyi itawapasa kushuhudia kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo.

1“Nimewaambia mambo haya yote ili msije mkaiacha imani. 2Watawatenga na masinagogi. Naam, saa yaja ambayo mtu ye yote atakayewaua atadhani kwa kufanya hivyo anamtumikia Mungu. 3Nao watawatenda haya kwa sababu hawamjui Baba wala mimi. 4Lakini nimewaambia ninyi mambo haya, ili saa hiyo ikiwadia mpate kukumbuka ya kuwa nilikuwa nimewaambia. Sikuwaambia mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi.

Kazi Ya Roho Mtakatifu

5“Sasa mimi ninakwenda kwake yeye aliyenituma, lakini hakuna hata aniulizaye, ‘Unakwenda wapi?’ 6Kwa sababu nimewaambia mambo haya, mioyo yenu imejawa na huzuni. 7Lakini amin nawaambia, yafaa mimi niondoke kwa kuwa nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu, lakini nikienda nitamtuma kwenu. 8Naye atakapokuja, atauthibitishia ulimwengu kuhusu dhambi, haki na hukumu. 9Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi, 10kwa habari ya haki, kwa sababu ninakwenda kwa Baba, nanyi hamtaniona tena, 11kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.
12“Bado ninayo mambo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili sasa. 13Atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonyesha mambo yajayo. 14Atanitukuza mimi, kwa maana atayachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi. 15Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu. Ndiyo maana nimesema Roho atachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi.
16“Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona.”

Huzuni Itageuka Kuwa Furaha

17Baadhi ya wanafunzi wakaulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona?’ Naye ana maana gani asemapo, ‘Kwa sababu ninakwenda kwa Baba?’ ” 18Wakaendelea kuulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Kitambo kidogo?’ Hatuelewi hilo analosema.”
19Yesu akatambua kuwa walitaka kumwuliza juu ya hilo, hivyo akawaambia, “Je, mnaulizana nina maana gani niliposema, ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona?’ 20Amin, amin nawaambia, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi. Ninyi mtahuzunika, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 21Mwanamke anapokuwa na utungu wa kuzaa huwa na maumivu kwa sababu saa yake imewadia. Lakini mtoto akiisha kuzaliwa, yule mwanamke husahau maumivu hayo kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtoto ulimwenguni. 22Hivyo ninyi mna maumivu sasa, lakini nitawaona tena, nayo mioyo yenu itafurahi na furaha yenu hakuna awaondoleaye. 23Katika siku hiyo hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin nawaambia, kama mkimwomba Baba jambo lo lote kwa Jina langu, yeye atawapa. 24Mpaka sasa hamjaomba jambo lo lote kwa Jina langu. Ombeni nanyi mtapewa, ili furaha yenu ipate kuwa kamili.

Amani Kwa Wanafunzi

25“Nimewaambia mambo haya kwa mafumbo. Saa yaja ambapo sitazungumza nanyi tena kwa mafumbo bali nitawaeleza waziwazi kuhusu Baba. 26Siku hiyo mtaomba kwa Jina langu. Wala sitawaambia kwamba nitamwomba Baba kwa ajili yenu, 27kwa maana Baba mwenyewe anawapenda, kwa sababu mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. 28Nilitoka kwa Baba na kuja ulimwenguni, sasa naondoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba.”
29Ndipo wanafunzi wake wakasema, “Sasa unazungumza waziwazi, wala si kwa mafumbo. 30Sasa tumejua kwamba wewe unajua mambo yote, wala hakuna haja ya mtu kukuuliza maswali. Kwa jambo hili tunaamini kwamba ulitoka kwa Mungu.”
31Yesu akawajibu, “Je, sasa mnaamini? 32Saa inakuja, naam, imekwisha kuwadia, mtakapotawanyika kila mmoja kwenda nyumbani kwake na kuniacha peke yangu. Lakini mimi si peke yangu kwa sababu Baba yu pamoja nami. 33Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”