Skip to content

Kumbukumbu la Torati 28:1 – 31:29

1Kama ukimtii BWANA Mungu wako kwa bidii na kufuata amri zake zote ninazokupa leo kwa bidii, BWANA Mungu wako atakuweka juu ya mataifa yote katika dunia. 2Baraka hizi zote zitakuja juu yako na kukupata, kama ukimtii BWANA Mungu wako:
3Utabarikiwa mjini na utabarikiwa mashambani.
4Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na mazao ya nchi yako na wanyama wako wachanga wa kufugwa, yaani ndama wa makundi yako ya ng’ombe, na wana-kondoo wa makundi yako.
5Kapu lako na vyombo vyako vya kukandia vitabarikiwa.
6Utabarikiwa uingiapo na utabarikiwa utokapo.7BWANA atasababisha adui wainukao dhidi yako kushindwa mbele yako. Watakujia kwa njia moja lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.
8BWANA ataagiza baraka juu ya ghala zako na juu ya kila kitu utakachogusa kwa mkono wako. BWANA Mungu wako atakubariki katika nchi anayokupa.
9BWANA atakufanya kuwa taifa lake takatifu, kama alivyokuahidi kwa kiapo, kama ukishika maagizo ya BWANA Mungu wako na kwenda katika njia zake. 10Kisha mataifa yote ya dunia wataona kuwa unaitwa kwa jina la BWANA, nao watakuogopa. 11BWANA atakupa kustawi kwa wingi, katika tunda la uzao wa tumbo lako, katika wanyama wachanga wa mifugo yako na katika mazao ya ardhi yako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwapa.
12BWANA atafungua mbingu, ghala zake za baraka, kukupa mvua kwa majira yake na kubariki kazi zako zote za mikono yako. Utakopesha mataifa mengi lakini hutakopa kwa ye yote. 13BWANA atakufanya kichwa, wala si mkia. Kama utazingatia maagizo ya BWANA Mungu wako ninayokupa siku hii ya leo na kuyafuata kwa bidii, daima utakuwa juu, kamwe hutakuwa chini. 14Usihalifu amri zangu zo zote ninazokupa leo, kwa kwenda kuume au kushoto, kwa kufuata miungu mingine na kuitumikia.

Laana Kwa Kutokutii

15Hata hivyo, kama hutamtii BWANA Mungu wako na kuzishika kwa bidii amri zake zote na maagizo ninayokupa leo, laana hizi zote zitakuja juu yako na kukupata:
16Utalaaniwa mjini na utalaaniwa mashambani.
17Kapu lako na chombo chako cha kukandia kitalaaniwa.
18Uzao wa tumbo lako utalaaniwa, mazao ya ardhi yako, ndama wa makundi yako ya ng’ombe na wana-kondoo wa makundi yako.
19Utalaaniwa uingiapo na utokapo.20BWANA ataleta laana juu yako, fadhaa na kukaripiwa katika kila kitu unachokigusa kwa mkono wako, mpaka uwe umeharibiwa na kuangamizwa ghafula kwa ajili ya maovu uliyoyafanya kwa kumwacha yeye. 21BWANA atakupiga kwa magonjwa mpaka akuangamize kutoka katika nchi unayoiingia kuimiliki. 22BWANA atakupiga kwa magonjwa ya kudhoofisha, kwa homa na kuwashwa, hari na kwa ukame, kutu na kuwa na uchungu ambavyo vitakupiga mpaka uangamie.
23Anga juu yako itakuwa shaba, na ardhi chini yako itakuwa chuma. 24BWANA atafanya mvua ya nchi yako kuwa mavumbi na mchanga; vitakujia kutoka angani mpaka uangamie.
25BWANA atakufanya ushindwe mbele ya adui zako. Utawajia kwa njia moja lakini utawakimbia mbele yao kwa njia saba, nawe utakuwa kitu cha kuchukiza kwa falme zote za dunia. 26Mizoga yenu itakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi, wala hapatakuwepo mtu ye yote wa kuwafukuza. 27BWANA atakupiga kwa majipu ya Misri na kwa vidonda vitokavyo usaha na kuwashwa, ambako huwezi kuponywa. 28BWANA atakupiga kwa wazimu, upofu na kuchanganyikiwa kwa akili. 29Wakati wa adhuhuri utapapasapapasa huko na huko kama mtu kipofu katika giza. Hutafanikiwa katika lo lote ufanyalo; siku baada ya siku utaonewa na kunyang’anywa, wala hakuna ye yote atakayekuokoa.
30Utaposa mke, lakini mtu mwingine atakutana naye kimwili. Utajenga nyumba, lakini hutaishi ndani yake. Utapanda shamba la mizabibu, lakini hutakula matunda yake. 31Ng’ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako lakini hutakula nyama yake. Punda wako atachukuliwa kwa nguvu kutoka kwako wala hatarudishwa. Kondoo wako watapewa adui zako, wala hakuna mtu ye yote wa kuwaokoa. 32Wanao na binti zako watatolewa kwa mataifa mengine, nawe utayachosha macho yako ukiwatazamia siku baada ya siku, hutakuwa na nguvu kuinua mkono. 33Taifa usilolijua watakula mazao ya nchi yako na taabu ya kazi yako, hutakuwa na cho chote, bali kuonewa kikatili siku zako zote. 34Vitu utakavyoviona kwa macho yako vitakufanya wazimu. 35BWANA atayapiga magoti yako na miguu yako kwa majipu yenye maumivu makali yasiyoponyeka, yakienea kutoka nyayo za miguu yako hadi utosini.
36BWANA atakupeleka wewe na mfalme uliyemweka juu yako uende kwenye taifa ambalo hukulijua wewe wala baba zako. Huko utaabudu miungu mingine, miungu ya miti na mawe. 37Utakuwa kitu cha kuchukiza, tena kitu cha kudharauliwa na kudhihakiwa kwa mataifa yote huko BWANA atakakokupeleka.
38Utapanda mbegu nyingi katika shamba lakini utavuna haba, kwa sababu nzige watazila. 39Utapanda mashamba ya mizabibu na kuyapalilia, lakini hutakunywa divai yake wala hutakusanya zabibu, kwa sababu wadudu watazila. 40Utakuwa na mizeituni katika nchi yako yote, lakini hutatumia hayo mafuta yake, kwa sababu zeituni zitapukutika. 41Utakuwa na wana na binti lakini hawatakuwa nawe, kwa sababu watachukuliwa mateka. 42Makundi ya nzige yatavamia miti yako yote na mazao ya nchi yako.
43Mgeni anayeishi miongoni mwako atainuka juu zaidi na zaidi kuliko wewe, lakini wewe utashuka chini zaidi na zaidi. 44Yeye atakukopesha, lakini wewe hutamkopesha. Yeye atakuwa kichwa, lakini wewe utakuwa mkia.
45Laana hizi zote zitakuja juu yako. Zitakufuatia na kukupata mpaka uangamizwe, kwa sababu hukumtii BWANA Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake aliyokupa. 46Zitakuwa ishara na ajabu kwako na kwa wazao wako milele. 47Kwa sababu hukumtumikia BWANA Mungu wako kwa furaha na kwa moyo wakati wa kufanikiwa kwako, 48kwa hiyo katika njaa na kiu, katika uchi na umaskini wa kutisha, utawatumikia adui ambao BWANA atawatuma dhidi yako. Yeye ataweka nira ya chuma shingoni mwako hadi amekwisha kukuangamiza.
49BWANA ataleta taifa dhidi yako kutoka mbali, kutoka miisho ya dunia, kama tai ashukiavyo mawindo chini, taifa ambalo hutaijua lugha yake, 50taifa lenye uso mkali lisilojali wazee wala kuwahurumia vijana. 51Watakula wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako mpaka umeangamia. Hawatakuachia nafaka, divai mpya au mafuta, wala ndama wo wote wa kundi lako au wana-kondoo wa kundi lako mpaka umekuwa magofu. 52Nao wataizingira miji yote katika nchi yako mpaka kuta ndefu za ngome ambazo unazitegemea zimeanguka. Watazingira miji yote katika nchi ambayo BWANA Mungu wako anakupa.
53Utakula uzao wa tumbo lako, nyama ya wana wako na binti zako ambao BWANA Mungu wako amekupa, kwa sababu ya mateso yale adui zako watakayokuletea wakati wa kukuzingira. 54Hata yule mtu mwungwana sana na makini miongoni mwako hatakuwa na huruma kwa ndugu yake mwenyewe au kwa mke ampendaye au watoto wake waliosalia, 55naye hatampa hata mmoja wao nyama ya watoto wake ambao anawala. Kwa kuwa hakuna kitu kingine kilichosalia kwake katika mazingiwa makali ambayo adui yako watakuletea kwa miji yako yote. 56Mwanamke ambaye ni muungwana sana na makini miongoni mwako, yaani ambaye ni makini sana na muungwana kiasi kwamba asingethubutu kugusa ardhi kwa wayo wa mguu wake, yeye atakuwa mchoyo kwa mume ampendaye na mwanawe mwenyewe au binti yake, 57kondoo la nyuma kutoka kwenye tumbo lake na watoto anaowazaa. Kwa kuwa anakusudia kuwala kwa siri wakati wa kuzingirwa na katika taabu zile ambazo adui yako atazileta juu yako na miji yako.
58Kama hutafuata kwa bidii maneno yote ya sheria hii, ambayo yameandikwa katika kitabu hiki na kama hutalicha hili jina la fahari na la kutisha, yaani la BWANA Mungu wako, 59BWANA ataleta mapigo ya kutisha juu yako na kwa wazao wako, maafa makali na ya kudumu, magonjwa mazito na ya kudumu. 60Atakuletea juu yako magonjwa yote ya Misri yale uliyoyaogopa, nayo yataambatana nawe. 61Pia BWANA atakuletea kila aina ya ugonjwa na maafa ambayo hayakuandikwa humu katika kitabu hiki cha sheria, mpaka utakapokuwa umeangamizwa. 62Ninyi ambao mlikuwa wengi kama nyota za angani mtaachwa wachache tu, kwa sababu hamkumtii BWANA Mungu wenu. 63Kama ilivyompendeza BWANA kuwafanya ninyi mstawi na kuongezeka kwa idadi, ndivyo itakavyompendeza kuwaharibu na kuwaangamiza ninyi. Mtang’olewa kutoka katika nchi mnayoiingia kuimiliki.
64Kisha BWANA atawatawanya miongoni mwa mataifa yote, kutoka mwisho mmoja wa dunia hadi mwingine. Huko mtaabudu miungu mingine, miungu ya miti na ya mawe, ambayo ninyi wala baba zenu hamkuijua. 65Miongoni mwa mataifa hayo hamtapata raha wala mahali pa kupumzisha wayo wa mguu wenu. Huko BWANA atawapa mahangaiko ya mawazo, macho yaliyochoka kwa kungojea na moyo uliokata tamaa. 66Utaishi katika mahangaiko siku zote, ukiwa umejaa hofu usiku na mchana, wala hutakuwa kamwe na uhakika wa maisha yako. 67Wakati wa asubuhi utasema hivi, “Laiti ingekuwa jioni!” Jioni utasema, “Laiti ingekuwa asubuhi,” kwa sababu ya hofu ile itakayojaza moyo wako na vitu vile macho yako yatakavyoviona. 68BWANA atawarudisha tena Misri kwa meli, safari niliyosema kamwe hamngeenda tena. Huko mtajiuza ninyi wenyewe kwa adui zenu kama watumwa wa kiume na wa kike, lakini hakuna ye yote atakayewanunua.

Yoshua Kutawala Baada Ya Mose

1Kisha Mose akaenda akasema maneno haya kwa Waisraeli wote: 2“Sasa nina miaka mia moja na ishirini nami siwezi tena kuwaongoza. BWANA ameniambia, ‘Hutavuka Yordani.’ 3BWANA Mungu wenu, yeye mwenyewe atavuka mbele yenu. Ataangamiza mataifa haya mbele yenu, nanyi mtaimiliki nchi yao. Pia Yoshua atavuka mbele yenu, kama BWANA alivyosema. 4Naye BWANA atawafanyia watu hao kile alichowafanyia Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, ambao aliwaangamiza pamoja na nchi yao. 5BWANA atawakabidhi kwenu, nanyi lazima mwatendee yale yote niliyowaamuru. 6Iweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa BWANA Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”
7Kisha Mose akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ile BWANA aliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao. 8BWANA mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”

Kusoma Sheria

9Kwa hiyo Mose akaandika sheria hii na kuwapa makuhani, wana wa Lawi, waliochukua Sanduku la Agano la BWANA na wazee wote wa Israeli. 10Kisha Mose akawaamuru, akasema: “Mwishoni mwa kila miaka saba, katika mwaka wa kufuta madeni, wakati wa Sikukuu ya Vibanda, 11Waisraeli wote wanapokuja mbele za BWANA Mungu wenu mahali atakapopachagua, utasoma sheria hii mbele yao masikioni mwao. 12Kusanya watu wote, wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili waweze kusikia na kujifunza kumcha BWANA Mungu wenu na kufuata kwa bidii maneno yote ya sheria hii. 13Watoto wao, ambao hawaijui sheria hii, lazima waisikie na kujifunza kumcha BWANA Mungu wenu kwa muda mtakaoishi katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”

Kuasi Kwa Waisraeli Kunatabiriwa

14BWANA akamwambia Mose, “Sasa siku ya kifo chako imekaribia. Mwite Yoshua, mkajihudhurishe katika Hema la Kukutania, mahali nitakapompa maagizo ya kazi.” Kwa hiyo Mose na Yoshua wakaja na kujihudhurisha kwenye Hema la Kukutania.
15Kisha BWANA akatokea katika Hema katika nguzo ya wingu, nalo wingu likasimama juu ya ingilio la Hema. 16Kisha BWANA akamwambia Mose: “Unakwenda kupumzika na baba zako, nao watu hawa hivi karibuni watazini na miungu migeni ya nchi wanayoingia. Wataniacha na kuvunja Agano nililofanya nao. 17Siku hiyo nitawakasirikia na kuwaacha; nitawaficha uso wangu, nao wataangamizwa. Maafa mengi na shida nyingi zitakuja juu yao, nao siku hiyo watauliza, ‘Je, maafa haya hayakuja juu yetu kwa sababu Mungu wetu hayuko pamoja nasi?’ 18Nami hakika nitauficha uso wangu siku hiyo kwa sababu ya maovu yao yote kwa kugeukia miungu mingine.
19“Sasa ujiandikie wimbo huu , uwafundishe Waisraeli na uwaamuru wauimbe, ili upate kuwa ushahidi wangu dhidi yao. 20Nitakapokwisha kuwaingiza katika nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi niliyowaahidi baba zao kwa kiapo, nao watakapokula wakashiba na kufanikiwa, watageukia miungu mingine na kuiabudu, wakinikataa mimi na kuvunja Agano langu. 21Maafa na shida zitakapokuja juu yao, wimbo huu utashuhudia dhidi yao, kwa sababu hautasahauliwa na wazao wao. Ninajua lile wanaloandaa kufanya, hata kabla sijawaingiza katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo.” 22Hivyo Mose akaandika wimbo huu siku ile na akawafundisha Waisraeli.
23BWANA akampa Yoshua mwana wa Nuni agizo hili: “Uwe hodari na shujaa, kwa kuwa utawaleta Waisraeli katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo, nami mwenyewe nitakuwa pamoja nawe.”
24Baada ya Mose kumaliza kuandika kwenye kitabu maneno ya sheria hii kutoka mwanzo hadi mwisho, 25akawapa Walawi wale waliolibeba Sanduku la Agano la BWANA agizo hili, akawaambia: 26“Chukueni Kitabu hiki cha Sheria mkakiweke kando ya Sanduku la Agano la BWANA Mungu wenu. Hapo ndipo kitakapokaa kama shahidi dhidi yenu. 27Kwa kuwa ninajua jinsi mlivyo waasi na mlivyo na shingo ngumu. Kama mmekuwa mkiasi dhidi ya BWANA nikiwa bado niko hai na nikiwa pamoja nanyi, mtaasi mara ngapi baada ya kufa kwangu! 28Kusanyeni mbele yangu wazee wote wa makabila yenu na maafisa wenu wote, ili nipate kusema maneno haya masikioni mwao na kuziita mbingu na nchi ili kushuhudia dhidi yao. 29Kwa kuwa ninajua baada ya kifo changu hakika mtakuwa waovu kabisa na kugeuka kutoka njia niliyowaamuru ninyi. Katika siku zijazo, maafa yatawapata kwa sababu mtafanya maovu mbele ya macho ya BWANA, na kuchochea hasira yake kwa yale mikono yenu itakayokuwa imefanya.”

Wimbo Wa Mose

30Mose akayasoma maneno ya wimbo huu kutoka mwanzo hadi mwisho katika masikio ya kusanyiko lote la Israeli: