Skip to content

Yohana 17

Yesu Ajiombea Mwenyewe

1Baada ya Yesu kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema:
“Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe.
 2Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa. 3Nao uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe uliye Mungu wa pekee, wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma. 4Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye. 5Hivyo sasa, Baba, unitukuze mbele zako kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ulimwengu haujakuwako.

Yesu Awaombea Wanafunzi Wake

6“Nimewajulisha jina lako wale ulionipa kutoka katika ulimwengu. Walikuwa wako, ukanipa mimi, nao wamelitii neno lako. 7Sasa wamejua ya kuwa vyote ulivyonipa vimetoka kwako, 8kwa kuwa maneno yale ulionipa nimewapa wao, nao wameyapokea na kujua kwamba kweli nimetoka kwako, nao wameamini kuwa wewe ulinituma. 9Ninawaombea wao. Mimi siuombei ulimwengu, bali nawaombea wale ulionipa kwa sababu wao ni wako. 10Wote walio wangu ni wako na walio wako ni wangu, nami nimetukuzwa ndani yao. 11Mimi sasa simo tena ulimwenguni, lakini wao bado wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba Mtakatifu, uwalinde kwa uweza wa jina lako ulilonipa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 12Nilipokuwa pamoja nao, niliwalinda, wakawa salama kwa lile jina ulilonipa. Hakuna hata mmoja aliyepotea, isipokuwa yule aliyekusudiwa, ili Maandiko yapate kutimia.
13“Lakini sasa naja kwako, nami ninasema mambo haya wakati bado nikiwa ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu kamili ndani yao. 14Nimewapa neno lako, nao ulimwengu umewachukia kwa kuwa wao si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu huu. 15Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu. 16Wao si wa ulimwengu huu, kama vile mimi nisivyo wa ulimwengu. 17Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndilo kweli. 18Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nawatuma vivyo hivyo. 19Kwa ajili yao najiweka wakfu ili wao nao wapate kutakaswa katika ile kweli.

Yesu Awaombea Wote Wamwaminio

20“Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao 21ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako, wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiye uliyenituma mimi. 22Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 23Mimi ndani yako na wewe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi.
24“Baba, shauku yangu ni kwamba, wale ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili waweze kuuona utukufu wangu, yaani, utukufu ule ulionipa kwa kuwa ulinipenda hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu.
25“Baba Mwenye Haki, ingawa ulimwengu haukujui, mimi ninakujua, nao wanajua ya kuwa umenituma. 26Nimefanya jina lako lijulikane kwao nami nitaendelea kufanya lijulikane, ili kwamba upendo ule unaonipenda mimi uwe ndani yao na mimi mwenyewe nipate kuwa ndani yao.”