Mfano Wa Wanawali Kumi
1“Wakati huo, Ufalme wa Mbinguni utakuwa kama wanawali kumi waliochukua taa zao na kwenda kumlaki bwana arusi. 2Watano wao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara. 3Wale wapumbavu walichukua taa zao lakini hawakuchukua mafuta ya akiba, 4lakini wale wenye busara walichukua taa zao na mafuta ya akiba kwenye vyombo. 5Bwana arusi alipokawia kuja wale wanawali wote wakasinzia na kulala.
6“Usiku wa manane pakawa na kelele: ‘Tazameni, huyu hapa bwana arusi! Tokeni nje mkamlaki!’
7“Ndipo wale wanawali wote wakaamka na kuzitengeneza taa zao. 8Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara, ‘Tupatieni mafuta yenu kidogo, taa zetu zinazimika.’
9“Lakini wale wenye busara wakawajibu, ‘Sivyo, hayatutoshi sisi na ninyi pia. Afadhali mwende kwa wauzao mkajinunulie mafuta yenu.’
10“Nao walipokuwa wakienda kununua mafuta, bwana arusi akafika. Wale wanawali waliokuwa tayari, wakaingia ndani pamoja naye kwenye karamu ya arusi na mlango ukafungwa.
11“Baadaye wale wanawali wengine nao wakaja, wakaita, ‘Bwana! Bwana! Tufungulie mlango!’
12“Lakini yeye bwana arusi akawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, siwajui ninyi!’
13“Kwa hiyo kesheni, kwa sababu hamjui siku wala saa.
Mfano Wa Watumishi Watatu Walioachiwa Talanta
14“Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama mtu anayetaka kusafiri, akawaita watumishi wake na kuweka mali yake kwenye uangalizi wao. 15Mmoja akampa talanta ▼ tano mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kila mmoja alipewa kwa kadiri ya uwezo wake. Kisha yeye akasafiri. 16Yule aliyepewa talanta tano akaenda mara moja akafanya nazo biashara akapata talanta nyingine tano zaidi. 17Yule aliyepewa talanta mbili akafanya vivyo hivyo, akapata nyingine mbili zaidi. 18Lakini yule mtumishi aliyekuwa amepokea talanta moja, alikwenda akachimba shimo ardhini na kuificha ile fedha ya bwana wake.
19“Baada ya muda mrefu yule bwana wa wale watumishi akarudi na kufanya hesabu nao. 20Yule mtumishi aliyepokea talanta tano akaja, akaleta nyingine tano zaidi. Akasema, ‘Bwana uliweka kwenye uangalizi wangu talanta tano. Tazama, nimepata faida talanta tano zaidi.’
21“Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache, nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’
22“Yule mwenye talanta mbili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, uliweka kwenye uangalizi wangu talanta mbili. Tazama nimepata hapa talanta mbili zaidi.’
23“Bwana wake akajibu, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu, umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache, nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’
24“Kisha yule mtumishi aliyepokea talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, nilijua kwamba wewe ni mtu mgumu, unayevuna mahali usipopanda na kukusanya mahali usipotawanya mbegu. 25Kwa hiyo niliogopa, nikaenda, nikaificha talanta yako ardhini. Tazama, hii hapa ile iliyo mali yako.’
26“Bwana wake akajibu, ‘Wewe mtumishi mwovu na mvivu! Ulijua kwamba ninavuna mahali nisipopanda na kukusanya mahali nisipotawanya mbegu. 27Vyema basi, ingekupasa kuweka fedha yangu kwa watoa riba, ili nirudipo, nichukue ile iliyo yangu na faida yake.
28“ ‘Basi mnyang’anyeni hiyo talanta mkampe yule mwenye talanta kumi. 29Kwa maana kila mtu mwenye kitu ataongezewa, naye atakuwa navyo tele. Lakini kwa mtu yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. 30Nanyi mtupeni huyo mtumishi asiyefaa nje, kwenye giza, mahali ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.’
Kondoo Na Mbuzi
31“Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. 32Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. 33Atawaweka kondoo upande wake wa kuume na mbuzi upande wake wa kushoto.
34“Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njoni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu, urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’
37“Ndipo wale wenye haki watakapomjibu wakisema, ‘Bwana, ni lini tulikuona una njaa tukakulisha au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha au ukiwa uchi tukakuvika? 39Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’
40“Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin, amin ninawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’
41“Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’
44“Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’
45“Naye atawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’
46“Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”