Skip to content

Yesu Awatokea Wanafunzi Wake

19Ikawa jioni ya ile siku ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walipokuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa Wayahudi, Yesu aliwatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi.” 20Baada ya kusema haya, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana.
21Yesu akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.” 22Naye alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. 23Mkimwondolea mtu ye yote dhambi zake, zitaondolewa na ye yote mtakayemfungia dhambi zake, zitafungiwa.”

Yesu Anamtokea Tomasi

24Lakini Tomasi, aliyeitwa Didimasi, yaani, Pacha, mmoja wa wale kumi na wawili, hakuwa pamoja nao Yesu alipokuja. 25Hivyo wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.”
Lakini yeye akawaambia, “Nisipoona zile alama za misumari mikononi mwake na kuweka kidole changu kwenye hizo alama za misumari na mkono wangu ubavuni mwake, sitaamini.”
26Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwa tena pamoja ndani ya nyumba, naye Tomasi alikuwa pamoja nao. Ndipo Yesu akaja milango ikiwa imefungwa na kusimama katikati yao akasema, “Amani iwe nanyi.” 27Kisha akamwambia Tomasi, “Weka kidole chako hapa na uone mikono yangu, nyosha mkono wako uguse ubavuni mwangu. Usiwe na shaka, bali uamini tu.”
28Tomasi akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!”
29Yesu akamwambia, “Umeamini kwa kuwa umeniona? Wamebarikiwa wale ambao hawajaona lakini wameamini.”

Kusudi La Kitabu Hiki

30Yesu alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki. 31Lakini haya yameandikwa ili mweze kuamini ya kuwa Yesu ndiye Kristo , Mwana wa Mungu na kwa kumwamini mpate uzima katika jina lake. John 20: 19-30

Yesu Awatokea Wanafunzi Saba

1Baada ya haya Yesu akawatokea tena wanafunzi wake kando ya Bahari ya Tiberia . Yeye alijionyesha kwao hivi: 2Simoni Petro, Tomasi aitwaye Didimasi, yaani Pacha, Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, wana wa Zebedayo na wanafunzi wengine wawili walikuwa pamoja. 3Simoni Petro akawaambia wenzake, “Mimi nakwenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Tutakwenda pamoja nawe.” Wakatoka, wakaingia ndani ya mashua, lakini usiku ule hawakupata cho chote.
4Mara baada ya kupambazuka, Yesu akasimama ufuoni, lakini wanafunzi hawakumtambua kwamba alikuwa Yesu.
5Yesu akawaambia, “Wanangu, je, mna samaki wo wote?”
Wakamjibu, “La.”
6Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu na tazama wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua.
7Yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia haya, akajifunga nguo yake kwa kuwa alikuwa uchi, naye akajitosa baharini. 8Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliyojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa 200 . 9Walipofika pwani, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake na mikate.
10Yesu akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.”
11Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu pwani. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa 153. Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika. 12Yesu akawaambia, “Njoni mpate kifungua kinywa.” Hakuna hata mmoja wao aliyethubutu kumwuliza, “Wewe ni nani?” Kwa sababu walijua ya kuwa ni Bwana. 13Yesu akaja, akachukua ule mkate, akawapa na vivyo hivyo akawagawia pia wale samaki. 14Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake tangu afufuke kutoka kwa wafu.

Yesu Amwuliza Petro Kama Anampenda

15Walipokwisha kula, Yesu akamwuliza Simoni Petro, “Je, Simoni mwana wa Yohana, unanipenda kweli kuliko hawa?”
Yeye akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”Yesu akamwambia, “Lisha wana-kondoo wangu.”
16Yesu akamwambia tena, “Simoni, mwana wa Yohana, wanipenda?”
Petro akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”Yesu akamwambia, “Chunga kondoo zangu.”
17Kwa mara ya tatu Yesu akamwuliza Petro, “Simoni mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akahuzunika sana kwa kuwa Yesu alimwuliza mara ya tatu, “Unanipenda?” Akamjibu, “Bwana, wewe unajua yote, unajua ya kuwa ninakupenda.”Yesu akamwambia, “Lisha kondoo zangu.
 18Amin, amin nakuambia, ulipokuwa kijana ulivaa na kwenda unakotaka, lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono yako na mtu mwingine atakuvika na kukupeleka usipotaka kwenda.” 19Yesu alisema haya ili kuashiria ni kifo cha aina gani Petro atakachomtukuza nacho Mungu. Kisha Yesu akamwambia Petro, “Nifuate!”
20Petro akageuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akiwafuata. (Huyu ndiye yule mwanafunzi aliyeegama kifuani mwa Yesu walipokula naye chakula cha mwisho na kuuliza, “Bwana, ni nani atakayekusaliti?”) 21Petro alipomwona huyo mwanafunzi, akamwuliza Yesu, “Bwana na huyu je?”
22Yesu akamjibu, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini? Wewe inakupasa unifuate!” 23Kwa sababu ya maneno haya ya Yesu, uvumi ukaenea miongoni mwa ndugu kwamba huyu mwanafunzi hangekufa. Lakini Yesu hakusema kuwa hangekufa. Yeye alisema tu kwamba, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini?”
24Huyu ndiye yule mwanafunzi anayeshuhudia mambo haya na ndiye ambaye ameandika habari hizi. Nasi tunajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli.
25Lakini kuna mambo mengine mengi ambayo Yesu alifanya. Kama yote yangeliandikwa, nadhani hata ulimwengu wote usingekuwa na nafasi ya kutosha kuweka vitabu vyote ambavyo vingeandikwa. Amen. (John 21: 1-25)

Ahadi Ya Roho Mtakatifu

1Katika kitabu changu cha kwanza nilikuandikia mpendwa Theofilo, kuhusu mambo yote Yesu aliyofanya na kufundisha tangu mwanzo, 2hadi siku ile alipochukuliwa kwenda mbinguni, baada ya kuwapa maelekezo kwa njia Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua. 3Baada ya mateso yake, alijionyesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu Ufalme wa Mungu. 4Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke humu Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake. 5Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku hizi chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”

Kupaa Kwa Yesu Kwenda Mbinguni

6Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamwuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”
7Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. 8Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”
9Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.
10Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao, 11wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.” (Acts 1:1-11)