Skip to content

Surat 2:67-73 (Ng’ombe)

Na Musa alipo waambia watu wake: Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mchinje ng’ombe. Wakasema: Je! Unatufanyia mzaha? Akasema: Audhubil lahi! Najikinga kwa Mwenyezi Mungu nisiwe miongoni mwa wajinga.

Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni ng’ombe gani? Akasema: Hakika Yeye anasema kwamba ng’ombe huyo si mpevu, wala si kinda, bali ni wa katikati baina ya hao. Basi fanyeni mnavyo amrishwa.

Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie nini rangi yake? Akasema: Yeye anasema, kuwa ng’ombe huyo ni wa manjano, na rangi yake imekoza, huwapendeza wanao mtazama.

Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni yupi? Hakika tunaona ng’ombe wamefanana. Na kwa yakini, Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda, tutaongoka.

Akasema: Yeye anasema: Kuwa huyo ni ng’ombe asiye tiwa kazini kulima ardhi wala kumwagia maji mimea, mzima, hana baka. Wakasema: Sasa umeleta haki. Basi wakamchinja, na walikaribia kuwa wasifanye hayo.

Na mlipo muuwa mtu, kisha mkakhitalifiana kwayo, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyatoa hayo mliyo kuwa mkiyaficha.

Tukasema: Mpigeni kwa kipande chake (huyo ng’ombe). Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anakuonyesheni Ishara zake ili mpate kufahamu.