Skip to content

Maji Ya Utakaso

1BWANA akamwambia Mose na Aroni: 2“Hivi ndivyo sheria ambayo BWANA ameagiza itakavyo: Waambie Waisraeli wakuletee mtamba mwekundu asiye na dosari wala waa na ambaye hajapata kufungwa nira. 3Mpeni kuhani Eleazari huyo mtamba; naye atatolewa nje ya kambi na kuchinjwa mbele yake huyo kuhani. 4Kisha kuhani Eleazari atachukua baadhi ya damu yake kwenye kidole chake na kuinyunyiza mara saba kuelekea upande wa mbele ya Hema la Kukutania. 5Wakati akali akitazama, mtamba huyo atateketezwa: ngozi yake, nyama yake, damu na sehemu zake za ndani. 6Kuhani atachukua kuni za mti wa mwerezi, hisopo na sufu nyekundu, na kuvitupa kwenye huyo mtamba anayeungua. 7Baada ya hayo, kuhani lazima afue nguo zake, na aoge mwili wake kwa maji. Kisha anaweza kurudi kambini, lakini atakuwa najisi kwa kawaida ya ibada mpaka jioni. 8Mtu amchomaye huyo mtamba lazima naye pia afue nguo zake na kuoga kwa maji, naye pia atakuwa najisi mpaka jioni.
9“Mtu ambaye ni safi atakusanya majivu ya mtamba huyo na kuyaweka mahali ambapo ni safi nje ya kambi kwa taratibu za kiibada. Yatahifadhiwa na jumuiya ya Kiisraeli kwa matumizi katika maji ya utakaso; ni kwa ajili ya kutakasa kutoka dhambini. 10Mtu akusanyaye majivu ya huyo mtamba ni lazima pia afue nguo zake, kadhalika naye pia atakuwa najisi hadi jioni. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa Waisraeli na kwa wageni wanaoishi miongoni mwao.
11“Mtu ye yote agusaye maiti ya mtu ye yote atakuwa najisi kwa siku saba. 12Ni lazima ajitakase mwenyewe kwa maji katika siku ya tatu na siku ya saba, ndipo atakuwa safi. Lakini kama hatajitakasa mwenyewe katika siku ya tatu na ya saba, hatakuwa safi. 13Mtu ye yote agusaye maiti ya mtu ye yote na kushindwa kujitakasa mwenyewe hunajisi Maskani ya BWANA. Mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na Israeli. Kwa sababu hajanyunyiziwa maji ya utakaso, yeye ni najisi; unajisi wake hubaki juu yake.
14“Hii ndiyo sheria itumikayo wakati mtu amekufa ndani ya hema: Ye yote aingiaye ndani ya hema hilo na ye yote aliye ndani yake watakuwa najisi kwa muda wa siku saba, 15nacho kila chombo kisicho na mfuniko juu yake kitakuwa najisi.
16“Mtu ye yote aliyeko nje mahali pa wazi agusaye mtu aliyeuawa kwa upanga au mtu aliyekufa kwa kifo cha kawaida, au mtu ye yote agusaye mfupa wa mtu aliyekufa au kaburi, atakuwa najisi kwa siku saba.
17“Kwa mtu aliye najisi, weka majivu ya sadaka ya utakaso wa dhambi ndani ya chombo, umimine maji safi juu yao. 18Kisha mtu aliye safi kwa kawaida za kiibada atachukua hisopo, achovye ndani ya maji, na kunyunyizia hema na vifaa vyote pamoja na watu ambao walikuwemo. Pia ni lazima amnyunyizie mtu ye yote ambaye amegusa mfupa wa mtu aliyekufa, au kaburi, au mtu ambaye ameuawa, au mtu ambaye amekufa kifo cha kawaida. 19Mtu ambaye ni safi ndiye atakayemnyunyizia ye yote ambaye ni najisi siku ya tatu na siku ya saba, na katika siku ya saba atamtakasa mtu huyo. Mtu ambaye ametakaswa lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji, na jioni ile atakuwa safi. 20Lakini ikiwa mtu ambaye ni najisi hakujitakasa mwenyewe, ni lazima akatiliwe mbali na jumuiya, kwa sababu ameinajisi Maskani ya BWANA. Maji ya utakaso hayajanyunyizwa juu yake, naye ni najisi. 21Hii ni sheria ya kudumu kwao.
“Mtu ye yote ambaye ananyunyiza yale maji ya utakaso lazima pia afue nguo zake, na ye yote ambaye hugusa maji ya utakaso atakuwa najisi mpaka jioni.
 22Kitu cho chote anachogusa mtu aliye najisi kitakuwa najisi, na ye yote akigusaye huwa najisi mpaka jioni.”