Skip to content

Ishara ya Lut – Qur’ani

Ishara ya Lutu – Taurati

Mwanzo 19

Surat 7:80-83 (The Heights)

80.Na tulimtuma Lut’, alipo waambia watu wake: Je, mnafanya uchafu ambao hajakutangulieni yeyote kwa uchafu huo katika viumbe vyote!

81. Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio mkwawacha wanawake? Kumbe nyinyi ni watu wafujaji!

82. Na haikuwa jawabu ya kaumu yake isipo kuwa kuambizana: Wafukuzeni katika mji wenu, maana hao ni watu wanao jitakasa.

83. Basi tukamwokoa yeye na watu wake, isipo kuwa mkewe, alikuwa miongoni mwa walio bakia nyuma.

84. Na tukawamiminia mvua. Basi tazama jinsi ulivyo kuwa mwisho wa wakosefu.

 Surat 11:77-83 (The Hud)

77. Na wajumbe wetu walipo kuja kwa Lut’ aliwahuzunukia na akawaonea dhiki. Akasema: Hii leo ni siku ngumu!

78. Wakamjia kaumu yake mbio mbio. Na kabla ya haya walikuwa wakitenda maovu. Yeye akasema: Enyi watu wangu! Hawa binti zangu, ndio wametakasika zaidi kwenu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi mbele ya wageni wangu. Hivyo, hamna hata mtu mmoja miongoni mwenu aliye ongoka?

79. Wakasema: Bila shaka umekwisha jua hatuna haki juu ya binti zako, na unayajua tunayo yataka.

80.Akasema: Laiti ningeli kuwa na nguvu kwenu, au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu!

81. (Wajumbe) wakasema: Ewe Lut’! Sisi ni wajumbe wa Mola wako Mlezi. Hawa hawatakufikia. Na wewe ondoka pamoja na ahali zako usiku ungalipo. Wala yeyote miongoni mwenu asitazame nyuma, isipo kuwa mkeo, kwani yeye utamfika msiba utakao wafika hao. Hakika miadi yao ni asubuhi. Je, asubuhi si karibu?

82.Basi ilipo fika amri yetu tuliigeuza nchi juu chini, na tukawateremshia mvua ya changarawe za udongo mgumu ulio kamatana wa Motoni,

83.Zilizo tiwa alama kwa Mola wako Mlezi. Na haya hayako mbali na wenye kudhulumu wengineo.

1Malaika wale wawili wakafika Sodoma wakati wa jioni, naye Loti alikuwa ameketi kwenye lango la mji. Wakati alipowaona, aliondoka kwenda kuwalaki na kuwasujudia hadi chini. 2Akasema, “Bwana zangu, tafadhali karibuni kwenye nyumba ya mtumishi wenu. Mnaweza kunawa miguu na kulala hapa kisha asubuhi na mapema mwendelee na safari yenu.”
Wakamjibu, “La hasha, tutalala hapa nje uwanjani.”
3Lakini akasisitiza kwa nguvu kwamba waingie pamoja naye nyumbani kwake. Akawaandalia chakula, mikate isiyotiwa chachu, nao wakala. 4Kabla hawajaenda kulala, watu wote kutoka kila sehemu ya mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, waliizunguka nyumba. 5Wakamwita Loti wakisema, “Wako wapi wale watu ambao walikuja kwako jioni hii? Watoe nje kwetu ili tuweze kuwalawiti.”
6Loti akatoka nje kuonana nao, akaufunga mlango nyuma yake, 7akasema, “La hasha, rafiki zangu. Msifanye jambo hili ovu. 8Tazama, ninao binti wawili ambao kamwe hawajakutana kimwili na mwanaume. Acha niwatoe nje kwenu, nanyi mnaweza kuwafanyia lo lote mnalotaka. Lakini msiwafanyie cho chote watu hawa, kwa sababu wako kwenye ulinzi chini ya dari langu.”
9Wakamjibu, “Tuondokee mbali.” Wakaendelea kusema, “Huyu mtu alikuja hapa kama mgeni na sasa anataka kuwa mwamuzi wetu! Tutakutenda vibaya kuliko wao.” Waliendelea kumlazimisha Loti na kusonga mbele ili kuvunja mlango.
10Lakini watu wale waliokuwa ndani wakanyoosha mkono wakamvuta Loti ndani ya nyumba na kufunga mlango. 11Kisha wakawapiga kwa upofu wale watu waliokuwa mlangoni mwa ile nyumba, vijana kwa wazee, hivyo hawakuweza kuupata mlango.
12Wale watu wawili wakamwambia Loti, “Una mtu mwingine ye yote hapa, wakwe zako, wana au binti, ama ye yote mwingine aliye wako katika mji huu? Waondoe hapa, 13kwa sababu tunapaangamiza mahali hapa. Kilio kwa BWANA dhidi ya watu wa hapa, ni kikubwa kiasi kwamba ametutuma kupaangamiza.”
14Kwa hiyo Loti alitoka ili kuzungumza na wakwe zake, waliokuwa wamewaposa binti zake. Akawaambia, “Fanyeni haraka kuondoka mahali hapa, kwa kuwa BWANA yu karibu kuangamiza mji huu!” Lakini wakwe zake walifikiri kwamba alikuwa akitania.
15Kunako mapambazuko, malaika wakawahimiza Loti, wakamwambia, “Fanya haraka! Mchukue mke wako na binti zako wawili walioko hapa, la sivyo utaangamizwa wakati mji utakapoadhibiwa.”
16Alipositasita, wale watu wakamshika mkono wake na mikono ya mke wake na binti zake wawili na kuwaongoza salama nje ya mji, kwa kuwa BWANA alikuwa na huruma kwao. 17Mara walipokwisha kuwatoa nje, mmoja wao akawaambia, “Mkimbie kwa usalama wenu! Msitazame nyuma, wala msisimame po pote katika tambarare! Kimbilieni milimani, ama sivyo mtaangamizwa!”
18Lakini Loti akawajibu, “La hasha, bwana zangu, tafadhalini! 19Mtumishi wenu amepata kibali mbele ya macho yenu, nanyi mmeonyesha wema mkubwa kwangu kwa kuokoa maisha yangu. Lakini siwezi kukimbilia milimani, janga hili litanikumba, nami nitakufa. 20Tazama, hapa kuna mji karibu wa kukimbilia, nao ni mdogo. Niruhusuni nikimbilie humo, ni mdogo sana, ama sivyo? Ndipo maisha yangu yatasalimika.”
21Akamwambia, “Vema sana, nitalikubali hili ombi pia, sitauangamiza mji ulioutaja. 22Lakini ukimbilie huko haraka, kwa sababu sitaweza kufanya lo lote mpaka ufike huko.” (Ndiyo maana mji huo ukaitwa Soari .)
23Wakati Loti alipofika Soari, jua lilikuwa limechomoza katika nchi. 24Ndipo BWANA akanyesha moto wa kiberiti juu ya Sodoma na Gomora, uliotoka mbinguni kwa BWANA. 25Hivyo akaiteketeza miji ile na eneo lote la tambarare, pamoja na wote waliokuwa wanaishi katika miji, hata pia mimea yote katika nchi. 26Lakini mke wa Loti akatazama nyuma, hivyo akawa nguzo ya chumvi.