Skip to content

Mathayo 5-7

Sifa Za Aliyebarikiwa

1Basi Yesu alipoona makutano, alipanda mlimani akaketi chini, nao wanafunzi wake wakamjia. 2Ndipo akaanza kuwafundisha, akisema: 3“Heri walio maskini wa roho,
maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao.
4Heri wale wanaohuzunika,
maana hao watafarijiwa.
5Heri walio wapole,
maana hao watairithi nchi.
6Heri wenye njaa na kiu ya haki,
maana hao watatoshelezwa.
7Heri wenye huruma,
maana hao watapata rehema.
8Heri walio na moyo safi,
maana hao watamwona Mungu.
9Heri walio wapatanishi,
maana hao wataitwa wana wa Mungu.
10Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki,
maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao.

11“Heri ninyi watu watakapowashutumu na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. 12Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kuu.

Chumvi Na Nuru

13“Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu cho chote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.
14“Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

Kutimiza Sheria

17“Msidhani kwamba nimekuja kufuta Torati au Manabii, sikuja kuondoa bali kutimiza. 18Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yo yote kutoka kwenye Torati mpaka kila kitu kiwe kimetimia. 19Kwa hiyo, ye yote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini ye yote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni. 20Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya walimu wa sheria na Mafarisayo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

Kuhusu Hasira

21“Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue, ye yote atakayeua atapaswa hukumu.’ 22Lakini mimi nawaambia kwamba, ye yote atakayemkasirikia ndugu yake wa kiume au wa kike, atapaswa hukumu. Tena, ye yote atakayemwambia ndugu yake wa kiume au wa kike, ‘Raca’ , yaani kumdharau na kumdhihaki, atapaswa kufanyiwa baraza. Lakini ye yote atakayesema ‘Wewe mpumbavu ulaaniwe!’ Atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.
23“Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, 24iache sadaka yako hapo, mbele ya madhabahu, uende kwanza ukapatane na ndugu yako wa kiume au wa kike, kisha urudi na ukatoe sadaka yako.
25“Patana na mshtaki wako upesi wakati uwapo njiani pamoja naye kwenda mahakamani, ili mshtaki wako asije akakutia mikononi mwa hakimu, naye hakimu akakutia mikononi mwa askari, nawe ukatupwa gerezani. 26Amin, nakuambia, hutatoka humo mpaka umelipa hadi senti ya mwisho.

Kuhusu Uzinzi

27“Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini’. 28Lakini mimi nawaambia kwamba, ye yote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. 29Jicho lako la kuume likikufanya utende dhambi, ling’oe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu. 30Kama mkono wako wa kuume ukikufanya utende dhambi, ukate uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu.

Kuhusu Talaka

31“Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu ye yote amwachaye mkewe na ampe hati ya talaka.’ 32Lakini mimi nawaambia, ye yote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na ye yote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa azini.

Kuhusu Kuapa

33“Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali timiza kiapo kile ulichofanya kwa Bwana.’ 34Lakini mimi nawaambia, Msiape kabisa, ama kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu, 35au kwa nchi, kwa kuwa ndipo mahali pake pa kuwekea miguu, au kwa Yerusalemu, kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu. 36Nanyi msiape kwa vichwa vyenu kwa kuwa hamwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37‘Ndiyo,’ yenu iwe ‘Ndiyo’ na ‘Hapana’, yenu iwe ‘Hapana.’ Lo lote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu.

Kuhusu Kulipiza Kisasi

38“Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ 39Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia, 40Kama mtu akitaka kukushtaki na kuchukua shati lako, mwachie achukue na koti pia. 41Kama mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili. 42Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.

Upendo Kwa Adui

43“Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ 44Lakini mimi ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, 45ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46Kama mkiwapenda wale wanaowapenda tu, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? 47Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo? 48Kwa hiyo iweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Kuwapa Wahitaji

1“Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.
2“Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 3Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, 4ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.

Kuhusu Maombi

5“Nanyi msalipo, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin, amin nawaambieni, wao wamekwisha kupata thawabu yao. 6Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako. 7Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao. 8Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba.
9“Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba:“ ‘Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako litukuzwe.
10Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike
hapa duniani kama huko mbinguni.
11Utupatie leo riziki zetu
za kila siku.
12Utusamehe deni zetu,
kama sisi nasi tulivyokwisha
kuwasamehe wadeni wetu.
13Usitutie majaribuni,
bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu
[kwa kuwa Ufalme ni wako na nguvu
na utukufu, hata milele. Amen].’

14Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe na ninyi pia. 15Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

Kuhusu Kufunga

16“Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonyesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupata thawabu yao kamilifu. 17Lakini mnapofunga, jipakeni mafuta kichwani na kunawa nyuso zenu 18ili kufunga kwenu kusionekane na watu wengine ila Baba yenu aketiye mahali pa siri, naye Baba yenu aonaye sirini atawapa thawabu yenu kwa wazi.

Akiba Ya Mbinguni

19“Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. 20Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. 21Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.

Jicho Ni Taa Ya Mwili

22“Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utakuwa na nuru. 23Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Kwa hiyo basi, kama nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza, hilo ni giza kuu namna gani!

Mungu Na Mali

24“Hakuna mtu ye yote awezaye kuwatumikia mabwana wawili, kwa kuwa ama atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau huyu mwingine. Ninyi hamwezi kumtumikia Mungu na Mali .

Msiwe Na Wasiwasi

25“Kwa hiyo nawaambia, msiwe na wasiwasi kuhusu maisha yenu: mtakula nini au mtakunywa nini, au kuhusu miili yenu, mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula na mwili zaidi ya mavazi? 26Waangalieni ndege wa angani, wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? 27Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake aweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake au kuongeza dhiraa moja  kwenye kimo chake?
28“Nanyi kwa nini kujitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29Lakini nawaambia, hata Mfalme Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa kama mojawapo ya hayo maua. 30Lakini ikiwa Mungu anayavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? 31Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ Au ‘Tutakunywa nini?’ Au ‘Tutavaa nini?’ 32Kwa maana watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kwamba mnahitaji hayo yote. 33Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake na haya yote mtaongezewa. 34Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.

Kuwahukumu Wengine

1“Usihukumu ili usije ukahukumiwa. 2Kwa maana kwa jinsi ile unavyowahukumu wengine, ndivyo utakavyohukumiwa na kwa kipimo kile utakachotoa ndicho utakachopokea.
3“Kwa nini unatazama kibanzi kidogo kilichomo kwenye jicho la ndugu yako na wala huoni boriti iliyoko kwenye jicho lako? 4Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Acha nitoe kibanzi kwenye jicho lako wakati kuna boriti kwenye jicho lako mwenyewe?’ 5Ewe mnafiki, toa kwanza boriti kwenye jicho lako mwenyewe, nawe ndipo utakapoona wazi ili kuondoa kibanzi kilichoko kwenye jicho la ndugu yako.
6“Msiwape mbwa vitu vilivyo vitakatifu, wala msitupie nguruwe lulu zenu. Kama mkifanya hivyo, watazikanyaga-kanyaga na kisha watawageukia na kuwararua vipande vipande.

Omba, Tafuta, Bisha

7“Ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 8Kwa maana kila aombaye hupewa, naye atafutaye huona, naye abishaye hufunguliwa mlango.
9“Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? 10Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka? 11Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua jinsi ya kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao? 12Kwa hiyo cho chote ambacho mnataka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Torati na Manabii.

Njia Nyembamba Na Njia Pana

13“Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa kupitia lango hilo. 14Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.

Mti Na Tunda Lake

15“Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa mwitu wakali. 16Mtawatambua kwa matunda yao. Je, watu huchuma zabibu kwenye miiba au tini kwenye michongoma? 17Vivyo hivyo, mti mwema huzaa matunda mazuri na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. 20Hivyo kwa matunda yao mtawatambua.

Mwanafunzi Wa Kweli

21“Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

Msikiaji Na Mtendaji

24“Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, lakini haikuanguka kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba. 26Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”
28Yesu alipomaliza kusema maneno haya, makutano ya watu wakashangazwa sana na mafundisho yake, 29kwa sababu alifundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wao wa sheria.